Sunday, 3 July 2016

Hii ndio kauli ya Makamu wa Rais Mh. Samia Suluhu kuhusu Viwanda vilivyopo nchini.

 TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania SAMIA SULUHU HASSAN ameviagiza viwanda vyote nchini kutumia msibomilia (BARCODES) za Tanzania kama hatua ya kuimarisha masoko na utambulisho wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na ya nje ya nchini.

Makamu wa Rais ametoa agizo hilo kwenye uzinduzi wa kampeni ya “NUNUA 620 Nunua Bidhaa za Tanzania” pamoja na Kusherekea miaka MITANO ya Taasisi ya Global Standard One –GSI-kwenye Viwanja wa Mwalimu Nyerere katika Maonyesho ya  40 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es salaam (SABASABA) mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali ya maonyesho.

Makamu wa Rais amesema matumizi ya BARCODES ni muhimu na ni ya lazima kwa sababu yanajumuisha taarifa nyingi ikiwemo asili ya bidhaa,jina la kampuni, kumbukumbu za uzalishaji,utunzaji,usafirishaji na usambazaji wa bidhaa.

Ameleeza kwamba itakuwa ni aibu kubwa kama katika masoko ya ndani ya nchi bado kutakuwa na bidhaa zinazotumia msibomilia (BARCODES) za nje na  kusisitiza kuwa matumizi ya Barcodes za Tanzania zitazuia na kupungua upotevu wa ajira kwa wataalamu wa ndani ya nchi.

Makamu wa Rais SAMIA SULUHU HASSAN amesema kuwa serikali ya awamu ya TANO ipo Tayari kufanya kazi na sekta binafsi katika kuleta mapinduzi makubwa yatakayosaidia kukuza uchumi wa taifa.

Kuhusu uanzishwaji wa Majukwa ya kumwezesha wanawake Kiuchumi  nchini, Makamu wa Rais amesema kuwa atahakikisha majukwaa hayo yanaleta matokeo chanya na yenye tija kwa wanawake Wakitanzania mijini na viijijini kwa kuwezeshwa kupata kupata elimu ya ujasiriamali,fursa za masoko,upatikanaji wa mikopo nafuu pamoja na elimu ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakwaza wanawake kiuchumi.

Makamu wa Rais pia ametoa wito maalum kwa wanawake kote nchini kujiunga na majukwaa hayo pindi yatakapoanzishwa kwenye maeneo yao kwa sababu yatakuwa na faida kubwa kwao kwa kuunganisha nguvukazi zao na kuzalisha bidhaa zenye ubora wa hali ya juu.

Imetolewa na
Ofisi ya Makumu wa Rais

No comments:

Post a Comment