Saturday 30 July 2016

Hii ndio kauli ya Rais Magufuli kuhusu kupiga mnada majengo ya serikali yaliyopo Dar es Salaam.

WAKATI suala la serikali kuhamia mkoani Dodoma likiwa dhahiri zaidi kila siku moja inayoongezeka, Rais John Magufuli ametangaza kuuza majengo ya wizara Dar es Salaam, mara atakapohamia yeye katika makao makuu hayo ya nchi.

Akizungumza jana kwenye mkutano wa hadhara mkoani Singida, katika siku ya kwanza ya ziara yake itakayomfikisha mikoa minne, Rais Magufuli alisema atahakikisha anauza baadhi ya majengo hayo kwa mnada, ili wale wasiotaka kuhama, wahame kwa lazima. Mbali na Singida, mikoa mingine atakayotembelea katika ziara hiyo aliyoanza jana ni Tabora, Shinyanga na Geita, ambako atazungumza na wananchi katika mikutano ya hadhara.

Katika mikutano hiyo, Rais Magufuli anatarajiwa kushukuru wananchi kwa kumpigia kura katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, na kueleza juhudi zinazofanywa na serikali kutatua kero zao na kuwaletea maendeleo.

Majengo mazuri Katika tangazo hilo, Rais Magufuli amesema majengo atakayoanza nayo, ni yale yanayotazama bahari; ambayo ndiyo mazuri zaidi, yenye mwonekano mzuri kutoka ofisini.

“Atakayeng’ang’ania kubaki huko, ajue hana kazi wala mshahara. Hatuwezi kuendelea kukaa miaka hamsini tunaimba tu kuhamia Dodoma, wakati hatutekelezi uamuzi wetu hadi wengine wameshatangulia mbele za haki,” alisema.

Alisema anajua akiitisha zabuni ya ofisi hizo, wateja watayakimbilia kwa wingi, hivyo wataong’ang’ania kubaki Dar es Salaaam, watakuwa wamejifukuzisha kazi wenyewe.

Uamuzi huo wa serikali kuhamia Dodoma japo ni wa siku nyingi na utekelezaji wake ulikuwa ukifanyika kidogokidogo kwa baadhi ya wizara na ofisi nyeti kujenga majengo yake katika mji huo, lakini hivi karibuni umepata kasi ambayo haijawahi kupatikana, baada ya Rais Magufuli kutangaza kuhakikisha serikali yote inahamia Dodoma kabla ya 2020.

Tamko hilo la Rais Magufuli lililotolewa wakati wa Mkutano Mkuu wa CCM wiki iliyopita na kurejewa katika Sikukuu ya Mashujaa mwanzoni mwa wiki hii, liliungwa mkono mara moja na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, ambaye alitangaza kuharakisha umaliziaji wa ujenzi wa nyumba yake, ili ahamie katika mji huo Septemba mwaka huu.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment