Saturday 30 July 2016

Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Muhongo afunguka haya kuhusu wanaotaka kulivamia Bomba la mafuta kutoka Uganda-Tanzania.

WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo  amewaonya wananchi wanaotaka kuvamia njia, litakapopita bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi katika bandari ya Tanga, kwa kujenga nyumba ili kulipwa fidia mradi utakapoanza.


Aliwaeleza kuwa bomba hilo lililopewa jina la East Africa Crude Oil Pipeline, watakaovamia wanapoteza fedha zao na itakula kwao, kwani watatumia ramani ya satelaiti iliyopigwa Juni mwaka jana, muda ambao mazungumzo ya ujenzi wa bomba hilo yalianza.

Akizungumza katika mkutano wa makatibu wakuu wa wizara zote pamoja na wakuu wa mikoa ambao bomba hilo linapita, Muhongo alieleza kuwa watu hao hawawezi kudanganya kwa lengo la kupata fedha wakidai kuwa bomba limewakuta.

Alisema kuna satelaiti 1007 zinazofanya utafiti duniani na mpaka Agosti mwaka jana, zilikuwa zote zikifanya kazi hivyo kuonesha ni majengo gani yalikuwepo katika njia hiyo, hivyo kutaka wananchi wapewe ramani inayoonesha bomba litakapopita ili kuepusha gharama.

Muhongo alisema leo atakutana na waziri wa Nishati wa Kongo kwa lengo la kujadiliana jinsi nchi hiyo itakavyoshirikishwa kwenye mradi huo mapema, huku akitarajia nchi ya Burundi kuungana katika mradi huo.

Alisema hatua hiyo itawezesha bomba hilo kutumiwa na nchi hizo kupitisha mafuta.

Burundi na Tanzania zinaendelea na utafiti katika ziwa Tanganyika na yakipatikana watatumia bomba hilo. Muhongo alisema pia wanatarajia kutumia bomba hilo kusafirisha mafuta kutoka Sudani kusini kutokana na kuwa ni rahisi kuyasafirisha mpaka Uganda na kutumia bomba hilo.

Bomba hilo la mafuta linatara kutumia Dola za Marekani bilioni 3.5 mpaka litakapokamilika na kutaka katibu mkuu kuunda kamati maalumu ya kudumu ambayo itakuwa na wajumbe wawili au watatu kutoka kila wizara kuhakikisha mradi huo unakamilika.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment