MAJENGO ya madarasa tisa, ofisi za walimu nne, maabara na vyoo katika shule ya sekondari Lindi, vimeteketea kwa moto, unaodaiwa kutokana na hitilafu ya umeme.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Renatha Mzinga aliwaambia waandishi wa habari kwamba moto huo ulianza saa 7 usiku wa kuamkia jana.
Alisema kikosi cha Zimamoto kilifika eneo la tukio, lakini kutokana na tatizo la kiufundi, walishindwa kufanya kazi ipasavyo.
Kwa mujibu wa kamanda, lililetwa gari la polisi lenye maji ambayo hutumika wakati wa kutuliza ghasia maarufu kama ‘washawasha’ likasaidia kazi ya kuzima moto, kabla ya kudhibitiwa kikamilifu asubuhi ya jana. Hata hivyo alisema wakati jamii ikihangaika kuzima moto huo, mmoja wa watu alikamatwa akidaiwa kuiba kompyuta mpakato.
Ingawa hakuna mtu aliyekufa, kamanda alisema vifaa mbalimbali vilivyokuwamo madarasani, ofisi za walimu na maabara, vimeteketea vyote.
Wananchi waliozungumzia ajali hiyo, walilalamikia utendaji wa kikosi cha Zimamoto kwa kusema si mzuri.
Kwa mujibu wa mashuhuda, gari la Zimamoto lilipofika, madarasa mawili ndiyo yaliyokuwa yameteketea lakini kutokana na kushindwa kuzima moto, uliendelea kusambaa na kuteketeza madarasa tisa, ofisi za walimu na vyoo.
Taarifa zilieleza kuwa jana, Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi, Selemani Jafo alikuwa njiani kuja mkoani hapa kuangalia tukio hilo.
No comments:
Post a Comment