Tuesday 26 July 2016

Mchungaji Lusekelo amkubali LOWASA na Kuipongeza UKAWA kwa kauli hii.

Mchungaji wa Kanisa la Maombezi (GRC) la Ubungo jijini Dar es Salaam, Anthony Lusekelo maarufu ‘Mzee wa Upako’ amesema kitendo cha viongozi wa CCM kulitaja zaidi jina la Edward Lowassa katika Mkutano Mkuu Maalumu wa chama hicho ni ishara kuwa Waziri Mkuu huyo wa zamani ni tishio.

“Nani! Lowassa…. jina lake kutajwa sana katika vikao vya CCM. Hiyo inaashiria kuwa ni mtu tishio. Ndiyo ni tishio,” alisema Lusekelo jana katika mkutano wake na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. 

Lusekelo ambaye hivi karibuni, Rais John Magufuli alishiriki ibada katika kanisa lake, alimzungumzia Lowassa baada ya kuulizwa swali juu ya mtazamo wake kuhusu Mkutano Maalumu wa CCM ambao jina la mgombea huyo wa urais kupitia Chadema na Ukawa lilitajwa na makada wengi wa chama hicho tawala. 

Alisema hilo lilidhihirika hata katika mchakato wa CCM kupata mgombea wake wa urais, kutokana na Lowassa kuungwa mkono kwa kiasi kikubwa. 

Alisema kitendo cha Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzua mjadala katika Mkutano Mkuu wa chama hicho tawala sambamba na wimbi la makada wanaohama vyama vyao, si mambo yanayopaswa kuwa mjadala kwa sababu uchaguzi ulishapita. 

Huku akisema: “Sizungumzi haya kwa ajili ya kujipendekeza, sihitaji ukuu wa wilaya,” Lusekelo aliwataka viongozi kukataa kuendeleza uhasama wa kisiasa na chuki kwa maelezo kuwa mwaka huu uwe maalumu kuzika tofauti hizo, kufanya kazi kulijenga Taifa na kuhubiri amani na umoja. 

Katika mkutano huo, Lusekelo alipongeza kuimarika kwa vyama vya upinzani akaponda mvutano ulioibuka bungeni akisema kukosa uzoefu kwa Naibu Spika, Dk Tulia Ackson kulichangia huku akiunga mkono kauli ya Rais kuzuia shughuli za siasa na kubainisha jinsi Rasimu ya Katiba ya Tume ya Jaji Joseph Warioba, ilivyopendekeza kupunguzwa kwa madaraka ya Rais.

Awapongeza wapinzani 
Akizungumzia nguvu ya vyama vya upinzani, Lusekelo alisema ushindani wa kisiasa umekuwa mkubwa kutokana na kuimarika kwa upinzani: “Chadema ya sasa si ile ya miaka ya 1990. Wanaongoza miji mikubwa na ukiona chama kina wabunge 40 usikipuuze. Hata nguvu ya mfalme ni watu.” 

No comments:

Post a Comment