MKURUGENZI wa Kampuni ya Farm Plant Limited, Mohamed Yusufali na wenzake wanne wamefikishwa mahakamani wakikabiliwa na mashitaka 199 ya utakatishaji wa fedha na kuisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh bilioni 15.
Mbali na Yusufali, washitakiwa wengine katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi ni viongozi wanaohusika katika usimamizi na uendeshaji wa Kampuni ya Superior Financing Solution Limited, Alloyscious Mandago, Isaack Kasanga, Taherali Taherali na Mohamed Kabula.
Washitakiwa wote walifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam na kusomewa mashitaka na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Shedrack Kimaro, akisaidiwa na Pius Hilla na Wakili Leonard Swai kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
Katika kesi hiyo, Yusufali ambaye aliingia mahakamani hapo akiburuza begi la nguo, anakabiliwa na mashitaka 196 ya kughushi, kuwasilisha nyaraka za uongo, kukwepa kulipa kodi na kuisababishia serikali hasara.Wengine wanakabiliwa na mashitaka matatu.
Akisoma shitaka la kwanza hadi la 30, Wakili Kimaro alidai kuwa katika tarehe tofauti tofauti kati ya mwaka 2008 hadi 2016, Yusufali anadaiwa kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwenye ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Alidai kuwa Yusufali alighushi hati 15 za usajili kuonesha kuwa kampuni 15 ikiwemo ya Festive General Business Limited, Cebers General Co Limited na Emi Gheneral Properties Limited zimesajiliwa kihalali, jambo ambalo si kweli.
Aidha, anadaiwa katika tarehe tofauti tofauti, Yusufali aliwasilisha nyaraka za uongo ambazo ni hati za kughushi kwenye Ofisi ya TRA Mkoa wa Kodi wa Kinondoni, akionesha kuwa kampuni hizo zimesajiliwa nchini kihalali na zinastahili kusajiliwa kama mlipa kodi.
Kimaro aliaendelea kudai katika shitaka la 31 na 32, kuwa Taherali na Kabula, wanadaiwa kughushi stakabali za malipo.
Akisoma shitaka la 33 hadi la 105, Wakili Swai alidai kuwa katika tarehe tofauti, Yusufali alighushi hati za stakabadhi za malipo kuonesha kuwa Kampuni ya Farm Plant ltd imenunua vifaa mbalimbali kutoka kwenye kampuni mbalimbali ikiwemo Value Builders & Electrical na Jamco Agencies.
Inadaiwa alighushi hati hizo kuonesha wamenunua vifaa kutoka kampuni mbalimbali ikiwemo ununuzi wa vifaa vyenye thamani ya zaidi ya Sh bilioni moja.
Katika shitaka la 106 hadi 196, ilidaiwa kuwa, katika tarehe tofauti tofauti, Yusufali alighushi nyaraka za malipo ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) ya kuanzia Februari 2008 hadi mwaka huu kuonesha Kampuni ya Farm Plant Ltd imenunua bidhaa zenye thamani mbalimbali katika kipindi hicho jambo ambalo si kweli.
Ilidaiwa katika shitaka la 107 kuwa, kati ya Januari, 2008 na Januari 2016, Dar es Salaam, Yusufali akiwa mkurugenzi anayehusika na masuala yanayohusu kampuni yake, iliyosajiliwa kama Mlipa Kodi Namba VRN 10-016040-Z aliwasilisha nyaraka za uongo kuhusu malipo yake ya kodi.
Ilidai kuwa aliwasilisha nyaraka hizo kwa Kamishna wa TRA na kukwepa kulipa kodi yenye thamani ya Sh 15,645,944,361.
Katika mashitaka mengine inadaiwa katika tarehe tofauti kati ya Machi 2011 na Januari 2016, Dar es Salaam, washitakiwa wote wakiwa wanahusika katika usimamizi na uendeshaji wa Kampuni ya Superior Financing Solution Ltd walifanya kosa la utakatishaji wa fedha.
Inadaiwa walifanya kosa hilo kwa kuficha uhalali, chanzo na mzunguko wa Sh 1,895,885,000 kwa kuzikopesha fedha hizo kwa watu mbalimbali na kupokea marejesho ya mikopo huku wakijua fedha hizo zimetokana na njia zisizo halali za kughushi na kukwepa kodi.
Aidha, Yusufali anadaiwa kati ya Januari 2008 na Januari mwaka huu, kwa vitendo viovu vya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo kwa Kamishna wa TRA, ameisababishia serikali hasar aya Sh bilioni 15.6 ambazo zilitakiwa kulipwa kama VAT.
Baada ya kusomewa mashitaka hayo kwa zaidi ya saa tatu, Hakimu Mkazi Mkuu Huruma Shahidi alisema kesi hiyo ni ya uhujumu uchumi hivyo washitakiwa hawatakiwa kujibu mashitaka hayo. Wakili Pius Hilla alidai wanaendelea na upelelezi wa kesi hiyo na kuiomba mahakama ipange tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi Julai 25, mwaka huu itakapotajwa tena. Washitakiwa wote walirudishwa rumande kwa kuwa kisheria mashitaka yanayowakabili hayana dhamana. Wanatetewa na jopo la mawakili likiongozwa na Hudson Ndusyepo, Martini Rwehumbiza, Richard Rweyongeza, Michael Ngallo na wengine
No comments:
Post a Comment