Tuesday, 26 July 2016

Taarifa Kamili kuhusu uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa juu ya mauaji ya Daudi Mwangosi.

MAHAKAMA Kuu Kanda ya Iringa imemtia hatiani askari Polisi, Pacificius Cleophace Simoni, kwa kosa la mauaji ya bila kukusudia ya mwanahabari Daudi Mwangosi yaliyotokea Septemba 2 mwaka 2012 katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Kwa mara ya kwanza Simoni alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12 mwaka 2012 akituhumiwa kufanya kwa kukusudia mauaji hayo wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari kwenye ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa Jamhuri umeilazimisha mahakama hiyo chini ya Jaji Kihwelo kuibadili kesi hiyo kutoka kwenye mauaji ya kukusudia na kuwa mauaji ya bila kukusudia ambayo hukumu yake ameisogeza mbele hadi kesho Jumatano.

Baada ya mabadiliko hayo, wakili wa upande wa Jamhuri, Adolph Maganga, aliiomba mahakama hiyo imhukumu mtuhumiwa huyo kifungo cha maisha jela kwa mujibu wa Kifungu cha 198 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu huku wakili wa utetezi, Lwezaula Kaijage akiiomba mahakama hiyo impunguzie adhabu kwa kumfunga kifungo cha nje.

Wakati akitetea hoja yake ya kuiomba Mahakama itoe adhabu ndogo ya kifungo cha nje kwa mtuhumiwa huyo, Lwezaula aliisihi mahakama hiyo imuonee huruma mtuhumiwa huyo kwa kosa alilolifanya bila kukusudia kwa sababu ni kijana mdogo mwenye miaka 27 anayetegemewa na Taifa kama nguvu kazi.

“Na alishiriki operesheni iliyosababisha maafa hayo bila ridhaa yake, amekaa mahabusu kwa miaka minne na katika kipindi hicho atakuwa amejutia sana kosa lake, amefiwa na wazazi wake wote wawili, ana wadogo zake watano wanaomtegemea na ana mke na mtoto mmoja mdogo,” alisema wakili huyo wakati akitoa ombi hilo.

Kwa msingi huo, wakili huyo alitumia Kifungu cha 38(11) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu Sura ya 16 kuomba Mahakama imhurumie mtuhumiwa huyo na kumfunga kifungo cha nje.

Akisoma maelezo ya kesi hiyo kabla ya kuibadili na kuwa na mauaji ya bila kukusudia, Jaji Kiwehlo alisema upande wa Jamhuri ulileta mashahidi wanne ambao kati yao watatu walitoa ushahidi ulioshindwa kuithibitishia moja kwa moja Mahakama kama mtuhumiwa huyo alikusudia alipofanya mauaji hayo.

Huku akishangaa kwa nini Jamhuri pamoja na kuwa na rasilimali za kutosha ilishindwa kuwaleta mashahidi wengine muhimu kama Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa wa wakati huo, Michael Kamuhanda na Ofisa Upelelezi wa Mkoa Wankyo, aliwataja mashahidi hao kuwa ni Said Mnuka, Azel Mwampamba na Lewis Obado ambao pia wote walikuwa askari Polisi wa vyeo tofauti.

Alisema ushahidi pekee uliomtia hatiani mtuhumiwa huyo ni ushahidi uliotolewa na shahidi namba tatu ambaye ni mlinzi wa amani, Flora Mhelela. 

Mlinzi huyo wa amani aliwasilisha mahakamani hapo ungamo la mtuhumiwa huyo lililomhusisha na mauaji hayo na ambalo wakati likiwasilishwa upande wa utetezi haukulikana pamoja na kwamba ulikuja kulikana baada ya ungamo hilo kuwasilishwa mahakamani hapo.

Kwa kupitia ungamo hilo ambalo Mahakama imejiridhisha bila shaka yoyote kwamba maelezo yake yalitolewa kwa hiari na mtuhumiwa huyo; mtuhumiwa huyo alikiri kuhusika na mauaji hayo japokuwa alisema yalikuwa ni ya bahati mbaya.

Sehemu ya ungamo hilo lililosomwa mahakamani hapo kwa mara nyingine tena na jaji huyo linasema; “Niliondoka kutoa msaada nikiwa na long range ambayo ni silaha inayotumika kupigia mabomu ya kishindo na machozi kama inavyoonesha katika gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012.”

“Pale katika eneo la tukio bila kujua wala kufikiria likafyatua bomu, likafunguka likamuua mwandishi Daudi Mwangosi na kumjeruhi OCS ambaye alikumbatiwa na marehemu, pia kuwajeruhi askari wengine watatu waliokuwa karibu yangu na marehemu.”

Watu mbalimbali walijitokeza kusikiliza kesi hiyo ni pamoja na Rais wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deo Nsokolo na Makamu Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deudatus Balile. 

Wengine waliojitokeza kuhudhuria kesi hiyo ni pamoja na wanaharakati wa haki za binadamu, wanahabari wa Mkoa wa Iringa na wananchi wa Manispaa ya Iringa.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment