MKE wa aliyekuwa bilionea maarufu jijini Arusha, marehemu Erasto Msuya, Miriam Msuya amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akikabiliwa na mashitaka ya kumuua dada wa bilionea huyo, Aneth Msuya.
Mshitakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi akiwa chini ya ulinzi mkali wa Jeshi la Polisi huku baadhi ya ndugu waliokuwa katika eneo la Mahakama wakilia.
Alisomewa mashitaka yake na Wakili wa Serikali Diana Lukondo mbele ya Hakimu Mkazi, Magreth Bankika. Wakili Diana alidai kuwa, Mei 25, mwaka huu katika eneo la Kibada, Kigamboni, Dar es Salaam, mshitakiwa alimuua Aneth Msuya ambaye ni wifi yake.
Mshitakiwa hakuruhusiwa kujibu mashitaka na kurudishwa rumande kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu, na pia kisheria mashitaka yanayomkabili hayana dhamana. Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hakimu Bankika aliahirisha kesi hiyo hadi Septemba 6, mwaka huu itakapotajwa tena.
Miriam alikamatwa wiki chache zilizopita nyumbani kwake Sakina mkoani Arusha na kusafirishwa hadi Dar es Salaam kwa ajili ya kusomewa mashitaka yanayomkabili.
Wakati bilionea Msuya aliuawa Agosti 7, 2013 kwa kupigwa risasi 22 wakati akiwa karibu na Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Ndege wa Kilimanjaro (KIA), Aneth aliuawa kwa kuchinjwa shingo akiwa nyumbani kwake Kibada, Kigamboni.
Aidha, kwa mujibu wa matukio yaliyokuwa yakiripotiwa Polisi tangu Erasto auawe, ndugu hao wamekuwa wakipatwa na matukio mfululizo likiwemo la dada yake, Antuja Msuya kumwagiwa dawa inayodaiwa kuwa ni sumu akiwa amelala chumbani, na Esther Msuya na mumewe Samuel Charles walinusurika kuuawa kwa kupigwa risasi wakiwa katika baa jijini Dar es Salaam.
USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment