Monday 1 August 2016

Hii ndio Taarifa kamili kuhusu Wauguzi 13 kutumbuliwa Mkoa Rukwa.

HALMASHAURI ya Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, imewaondoa wauguzi 13 kwenye orodha ya malipo baada ya kubainika kuwa wana vyeti feki.


 Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo, limemfukuza kazi na kumtoa kwenye orodha ya malipo mhudumu wa zahanati iliyopo kijijini Mkombo, Winfrida Ngulo baada ya kukiri kuwa vyeti alivyokuwa navyo ni feki.

Pia madiwani wameagiza muuguzi Daraja la Pili aliyekuwa akifanya kazi kwenye zahanati hiyo ya Mkombo, Fatuma Efanga anayetuhumiwa kutoroka na zaidi ya Sh 700,000 zikiwa ni michango ya Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF) zilizochangwa na kaya maskini ili wahudumiwe kwenye zahanati hiyo.

Muuguzi huyo inadaiwa alikimbia na fedha hizo baada ya kubainika kuwa na vyeti feki.

Baraza hilo lililazimika kukaa kama kamati ili kumjadili na kumtolea maamuzi mhudumu huyo Ngulo ambaye inadaiwa alipofikishwa mbele ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) alikiri kuwa na vyeti feki .

Awali akichangia kwenye kikao cha baraza hilo, Diwani Mwachusa Sinjela alitahadharisha kuwa watumishi hewa na wenye vyeti feki wakipata taarifa kuwa wamebainika wamekuwa wakitoroka na kusababisha hasara.

“Mfano ninao kuna mtumishi wa afya (Fatuma) kwenye kata yangu nimepata taarifa kuwa ametoroka kituoni na fedha za michango ya CHF kiasi cha Sh 700,000 na hajulikani alikojificha,” alidai Sinjela.

Kaimu Mganga Mkuu wa Wilaya ya Kalambo, Dk Arcado Mwamba alisema orodha yote ya kaya maskini waliochanga fedha hizo CHF ipo na inafahamika. Kwa mujibu wa Dk Mwamba, zahanati hiyo ya Mkombo ilikuwa na watumishi wawili tu, Efanga na Ngulo ambao walikuwa wakitoa huduma.

“Kwa mantiki hiyo, zahanati hiyo kwa sasa haina mhudumu yeyote wa afya ila tuko mbioni kuwapeleka huko wahudumu wengine wa afya,” alieleza Dk Mwamba.

Akizungumza na gazeti hili nje ya baraza hilo, Ofisa Utumishi na Utawala wa halmashauri hiyo, John Maholani alisema wauguzi wa afya 13 wameondolewa kwenye orodha ya malipo baada ya kubainika kuwa wana vyeti feki.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment