Thursday 11 August 2016

Maamuzi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi kuhusu dhamana kwa mwizi wa Milioni 7 Kwa Dakika .

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imetupilia mbali maombi ya kufutwa kwa shitaka la utakatishaji fedha katika katika kesi ya kuisababishia serikali hasara ya Sh bilioni 14 inayomkabili, mfanyabiashara Mohammed Yusufali ‘Choma’ na mwenzake.
 
Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri alitoa uamuzi huo jana baada ya kupitia hoja zilizowasilishwa na pande zote mbili katika kesi hiyo.

 Kutokana na uamuzi huo, washitakiwa wataendelea kusota rumande hadi kesi itakapokwisha kwa kuwa kisheria mashitaka ya utakatishaji wa fedha hayana dhamana.
 
Katika kesi hiyo Choma aliyewahi kutajwa kujipatia Sh milioni saba kwa dakika moja kwa njia ya udanganyifu katika mapato ya serikali, pamoja na mfanyabiashara Samuel Lema, wanakabiliwa na mashitaka 222 ya kula njama, kutakatisha fedha, na kuisababishia serikali hasara hiyo kwa kukwepa kulipa kodi.
 
Akitoa uamuzi huo, Hakimu Mashauri alisema Mahakama imetupilia mbali maombi hayo yaliyowasilishwa na upande wa utetezi kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.
 
Alisema mahakama inakubali kuwa hati ya mashitaka inayowahusu washitakiwa hao haina makosa, hivyo Mahakama haiwezi kubadili hati hiyo kwa kuwa haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.
 
Aidha aliongeza kuwa, kama upande wa utetezi ungekuwa na nia ya kutaka kufutwa kwa shitaka hilo ungewasilisha maombi hayo tangu awali. Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 18, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa.
 
Katika hoja za ombi hilo, Wakili wa utetezi Alex Mgongolwa aliomba shitaka hilo kufutwa kwa kuwa lina mapungufu kisheria na kuongeza kuwa si kila kosa la wizi na kughushi ni utakatishaji fedha, bali makosa yanayofuata baada ya vitendo hivyo yaani kuficha chanzo au asili ya upatikanaji wa fedha hizo ndiyo kosa la utakatishaji.
 
Alidai maelezo ya kwenye shitaka la 221 hayajengi kosa la utakatishaji fedha hivyo aliiomba mahakama ifute shitaka hilo ili waendelee na mashitaka mengine.
 
Upande wa Jamhuri uliiomba mahakama itupilie mbali ombi hilo kwa kuwa halina msingi kisheria na shitaka hilo lina maelezo ya kutosha kujenga kosa la utakatishaji wa fedha.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUTU FOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment