Tuesday, 23 August 2016

Mpango Milioni 50 kila kijiji za Rais Magufuli zafikia hapa

BARAZA la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), limesema mpango wa utekelezaji wa ahadi ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mitaa, maarufu kama Mabilioni ya Rais John Magufuli, umeiva.

Mpango huo uliobatizwa jina la Fedha za Mfuko wa Mzunguko, unalenga kukabiliana na tatizo la mitaji kwa ajili ya kuendesha shughuli za kiuchumi kwa wananchi wanaoishi maeneo ya mijini na vijijini.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Beng’i Issa alisema Dar es Salaam jana kuwa fedha hizo zimelenga kukopesha vikundi vya wajasiriamali kupitia Vyama vya Ushirika vya Akiba na Mikopo (Saccos) na vikundi vya kifedha vya kijamii vikiwemo Vicoba, kwa ajili ya kuanzisha au kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Alisema hivi karibuni kumekuwa na taarifa kutoka sehemu mbalimbali nchini kuwa kuna baadhi ya taasisi na watu binafsi, wanawadanganya wananchi kuwa fedha hizo zitapitia kwenye taasisi zao na kuwataka wananchi kujisajili nao ili waweze kufaidika na fedha hizo, jambo ambalo si la kweli.

“Watu na taasisi hizo zinazowadanganya wananchi zimekuwa zikiwatoza viwango mbalimbali vya fedha kwa kile wanachodai ni ada ya usajili ili vikundi hivyo vya wananchi viweze kusajiliwa na kutambuliwa kuweza kufaidika na mamilioni hayo kwa kila kijiji,” alisema.

Aidha alisema watu hao wenye nia ovu, wamekuwa wakidai wametumwa na Baraza hilo la NEEC, kuwaandaa wananchi waweze kufaidika na mpango huo wa serikali.

“Kutokana na hali hiyo, NEEC tunapenda kutoa taarifa kwa umma kuwa hatujatuma mtu binafsi au taasisi yoyote kwenda kwa wananchi kuahidi jambo lolote kuhusu Mpango wa Milioni 50 kwa kila kijiji. “Hivyo kama kuna mtu binafsi au taasisi itakayobainika kuwadanganya wananchi taarifa itolewe kwa vyombo vya dola ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja,” alisema.

Alisema serikali ipo mbioni, kukamilisha utaratibu wa utekelezaji wa mpango huo na mara utakapokamilika, taarifa itatolewa kwa umma kupitia vyombo vya habari na viongozi wa serikali katika ngazi mbalimbali nchini. Alisema taarifa itakayotolewa itafafanua kuhusu utaratibu wa kuwafikia walengwa wa mpango huo, na kusisitiza kuwa maandalizi yamekamilika.

USISAHAU KULIKE NA KUSHARE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPA ULIPO.ASANTE

No comments:

Post a Comment