Friday 18 November 2016

Mahakama yatoa maamuzi kuhusu dhamana ya Godbless Lema.


Hatma ya dhamana ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), ilishindwa kujulikana jana baada ya mawakili wa Serikali kuweka pingamizi, wakipinga Mahakama Kuu, Kanda ya Arusha kusikiliza maombi ya dhamana yaliyowasilishwa na mawakili wa mshtakiwa.

Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Jaji Sekela Moshi, alisema   kutokana na pingamizi hiyo, atasikiliza hoja za sheria zilizowasilishwa mahakamani hapo kabla hajatoa uamuzi wowote juu ya dhamana ya mshtakiwa.

Aliwaelekeza mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha hoja za sheria kabla mahakama haijaendelea na hatua yoyote.

Jaji Moshi alisema atatoa uamuzi kuhusu mvutano huo wa sheria,  Novemba 22, mwaka huu

Katika maombi hayo namba sita ya mwaka 2016, Jamhuri iliwakilishwa na mawakili, Matenus Marandu na Paul Kadushi wakati Lema anatetewa na jopo la mawakili sita ambao ni Peter Kibatala, John Mallya, Adam Jabir, Sheck Mfinanga, Faraji Mangula na Charles Adiel.

Katika shauri hilo jana, hoja za sheria za pingamizi zilianza kusikilizwa saa 4:54 asubuhi hadi saa 7:25 mchana ambako mawakili wa Serikali na wale wa upande wa utetezi, walichuana vikali kujenga hoja.

Akiwasilisha pingamizi hilo, wakili Kadushi, aliiomba mahakama iwaruhusu kuwasilisha pingamizi moja na kama mahakama ikishindwa kuridhia pingamizi hilo, wawasilishe pingamizi la pili.

Alidai   maombi hayo yaliyosainiwa na wakili Kibatala yanalenga katika kifungu cha 372 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai kinachoipa Mahakama Kuu kufanya mapitio ya mashauri ya kesi za mahakama za chini.

Hoja ya sheria inasema   mabadiliko ya sheria yaliyofanyika mwaka 2002 yaliondosha haki za pande zote katika kesi za jinai kuomba rufaa au mapitio ya uamuzi mdogo uliofanywa katika mahakama zinazoongozwa na mahakimu nchini.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 43 (2) cha sheria ya mahakama za mahakimu, maombi hayo yanakinzana na kifungu hicho kwani uamuzi huo mdogo unaopingwa na mawakili wa mshtakiwa, haujamaliza shauri la jinai.

“Lakini pia, uamuzi huo unaobishaniwa na mawakili wa mshtakiwa, uko katika ukurasa wa 17 hadi 19, hivyo mahakama inafungwa na sheria kusikiliza rufaa au mapitio katika uamuzi mdogo.

“Kwa kuwa uamuzi ni mdogo mahakama inakuwa na uamuzi wa kutupilia mbali maombi haya na kusubiri tuendelee na mwenendo wa kesi. Lakini, kama mahakama haitavutiwa au kushawishiwa  na hoja hii, tunaomba kutoa hoja ya pili,”alidai wakili Kadushi

Baada ya hatua hiyo, hoja ya pili iliwasilishwa ikisema maombi ya Lema hayajakidhi matakwa ya sheria, kifungu cha 359 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, sura ya 20 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2,002.

Kwa mujibu wa wakili Kadushi, kifungu hicho kinaelekeza namna mtu asiporidhika na uamuzi uliotolewa na mahakama ya chini, anavyotakiwa kukata rufaa mahakama kuu.

“Msingi wa sheria umeshawekwa na mahakama kuwa maombi ya kufanya mapitio kamwe siyo mbadala wa rufaa na uamuzi mwingi umetamka hivyo,” alidai wakili Kadushi.

Katika maelezo yake, wakili huyo alirejea mashauri mbalimbali ya Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa yenye kesi za namna hiyo na kudai kuwa kulikuwa na haki ya waleta maombi kukata rufaa na haki hiyo ipo mpaka sasa.

USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE

                              SUBSCRIBE ON YOUTUBE TIKISA TV

No comments:

Post a Comment