Tuesday, 8 November 2016

Mwenyekiti wa Klabu ya Azam, Said Mohammed afariki dunia.

Uongozi wa Klabu ya Azam FC kwa masikitiko makubwa, unatangaza kifo cha mwenyekiti wake, Mzee Said Mohamed Abeid, kilichotokea alasir ya  Novemba 7, 2016, katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam.

Mzee Said Mohamed, atakumbukwa kama mmoja wa nguzo muhimu kwenye mafanikio ya klabu ya Azam FC tangu kuanzishwa kwake miaka takribani nane iliyopita.

Chini ya uongozi wake kama mwenyekiti wa Azam FC, aliiongoza klabu hii kunyakuwa mataji mbalimbali makubwa na kwa mafanikio, ikiwemo taji la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Mapinduzi mara mbili pamoja na Ngao ya Jamii.

Si hivyo tu, mchango wake Mzee Said Mohamed hauku-ishia nyumbani kwake Azam FC tu, bali hata kwenye familia ya soka la Tanzania kwa ujumla wake ambapo hadi umauti unamkuta alikuwa ni makamu mwenyekiti wa bodi ya ligi kuu Tanzania bara na mjumbe wa kamati mbalimbali za shirikisho la soka Tanzania, TFF.

Sisi Azam FC, tutamkumbuka Mzee Said Mohamed kwa ucheshi wake, ukarimu na uchapakazi wake kwa ujumla.

Marehemu alizaliwa tarehe 20 Machi 1940 visiwani Zanzibar na anatarajiwa kuzikwa Jumanne leo  tarehe 8 Novemba, 2016 kwenye makaburi ya Kisutu baada ya swala ya Alasir, mwili wake utaswaliwa kwenye msikiti wa Maamour Upanga.

Mwenyezi Mungu ailaze roho yake Said Mohamed Abeid mahali pema peponi, Amiin,

Innalilah Wa-inna-ilaih Rajioun.

Nassor Idrissa,

Makamu Mwenyekiti,

Azam Football Club.

No comments:

Post a Comment