Siku tatu baada ya Rais John Magufuli kueleza bayana kwamba suala la Katiba Mpya si kipaumbele chake kwa sasa akitaka aachwe ili ainyooshe nchi kwanza, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu amesema kiongozi huyo hawezi kunyoosha nchi bila kuwa na Katiba Mpya iliyotokana na maoni ya wananchi.
Wakati Lissu akisema hayo, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Damiani Lubuva amesema atatolea ufafanuzi suala hilo siku za karibuni.
Lubuva na Lissu walieleza hayo walipotakiwa kuzungumzia kauli ya Rais Magufuli kwamba kipaumbele chake ni kuchapa kazi ili kuinyoosha nchi na mengine yafuate ikiwamo Katiba Mpya.
Magufuli alitoa kauli hiyo Novemba nne, alipozungumza na Wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari siku moja kabla ya kutimiza mwaka mmoja tangu aingie madarakani.
Lakini, Lissu alisema nchi haiwezi kunyooka bila kunyoosha kwanza Katiba inayoiongoza ambapo alipendekeza uwepo wa Katiba Mpya badala ya kuifanyia marekebisho iliyopo sasa.
“Tulishaondoka kwenye mjadala wa kuziba viraka kwenye Katiba, tumeshakubaliana kwamba tunahitaji mabadiliko ya Katiba yote si sehemu tu. Rais asidhani mtu akikalia kiti hicho basi neno lake ni sheria ya nchi. Haiwezekani,” alisema.
Alisema mchakato wa Katiba Mpya hautakiwi kuendelea ulipoishia kwa maelezo kuwa ikiwa hivyo nchi haiwezi kufika popote.
“Katiba Inayopendekezwa ni kama imepakwa rangi ya Katiba ya sasa. Inaonekana mpya lakini misingi yake ni ya Katiba ya sasa…, kama Rais Magufuli anataka kunyoosha nchi, anapaswa kuirejea Rasimu ya Jaji Warioba. Tuanzie hapo, zaidi ya hivyo atajidanganya na kuwadanganya Watanzania,” alisema.
Lissu ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alisema nchi haiwezi kuongozwa kwa matamko ya kiongozi mkuu pekee bila kuangalia matatizo ya kisheria.
“Anafikiri akiamua yeye kama Rais unafuata utekelezaji? Kuna matatizo mengine ya kikatiba…, hayawezi kubadilika bila kufanyika kwa mabadiliko ya Katiba. Kuna mambo ili yanyooke ni lazima uwe na Katiba nzuri. Usipoyashughulikia hayo mengine yote hayatawezekana,”alisema Lissu.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ,Jaji Lubuva alipoulizwa kuhusu mchakato wa Katiba Mpya na kauli ya Rais Magufuli alisema suala hilo linahitaji kukaa na kulizungumza vizuri.
“Naomba upokee kuwa nimekuelewa ila kwa sasa ninachoweza kusema nitatoa ufafanuzi mzuri kuhusu suala hilo kwani ni jukumu la ofisi yangu,” alisema.
Alisema ni kweli baada ya Katiba Inayopendekezwa kupigiwa kura na Bunge hatua iliyokuwa inafuata ilikuwa ni kuitisha Kura ya Maoni, lakini ilishindikana kutokana na kuingiliana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Kabla ya Rais Magufuli kutoa kauli yake kuhusu Katiba Mpya, siku za karibuni NEC iliwahi kueleza kwamba ipo katika hatua mbalimbali za kuhakikisha mchakato huo unafanyika kwa mujibu wa sheria.
Katika kauli yake ya Novemba nne, Rais Magufuli alisema wakati anaomba kura hakuweza kuzungumzia Katiba hivyo kwa sasa kilichopo mbele yake ni kunyoosha nchi kwanza na Katiba mpya itakuja baadaye.
USISAHAU KULIKE NA KU-SHARE NA KU-LIKE PAGE YETU FACEBOOK TIKISA MEDIA KUFOLLOW TWITTER @TIKISA MEDIA NA INSTAGRAM TIKISA ENTERTAINMENT MEDIA ILI HABARI ZOTE KUBWA ZIKUFIKIE HAPO ULIPO.ASANTE
No comments:
Post a Comment