Sunday 20 November 2016

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atoa siku 18 kwa mkandarasi wa umeme kufikisha kiwandani.

Image result for majaliwa kassimu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa siku 18 kwa mkandarasi wa umeme kwenye kiwanda cha Kiluwa Steel Group awe amemaliza kazi ya kuweka umeme mkubwa ili kiwanda hicho kianze kazi.

Ametoa agizo hilo  wakati akizungumza na wananchi na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Pwani waliofika kiwandani hapo eneo la Mlandizi wakati akikagua utekelezaji wa maagizo aliyoyatoa Julai 12, mwaka huu alipozuru kiwanda kwa mara ya kwanza.

"Nilipokuwa hapa mara ya kwanza niliagiza itengenezwe njia ya reli kutoka njia panda ya reli ya kati, lakini pia niliagiza uwekwe umeme wa msongo mkubwa ili kiwanda kiweze kuanza uzalishaji mapema mwakani. Nimefarijika kukuta maagizo haya yametekelezwa kwa kiasi kikubwa isipokuwa hili la umeme.

"Mkandarasi ameomba siku 14, nimempa hadi tarehe 7 Desemba ahakikishe umeme unafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa. Sasa hivi wameanza test lakini itachukua muda ili transfoma iweze kuhimili mzigo mkubwa... hili ni suala la kitaalamu kwa hiyo tuwape muda."

Waziri Mkuu pia alisema amefarijika kusikia kuwa orodha ya watu wanaodai fidia sababu ya kupisha njia ya reli ijengwe, imeshawasilishwa kwa Mkuu wa Mkoa na mwenye kiwanda yuko tayari kuwalipa mara taratibu zitakapokamilika.

Waziri Mkuu alitoa agizo kwa Naibu Katibu Mkuu wa Viwanda na Biashara, John Malongo awasiliane na Wizara ya Nishati na Madini ili afuatilie ni kwa nini watengenezaji wa makaa ya mawe hawafuati vipimo halisi vinavyotolewa na wawekezaji.


No comments:

Post a Comment