Thursday 1 December 2016

Askari magereza walalamikia rushwa na ufisadi, ulazimika kutoa rushwa ili kupata sare.

Image result for RAIS MAGUFULI MAGEREZA UKONGA
Hivi karibuni Rais John Magufuli alipiga marufuku Jeshi la Magereza na majeshi mengine nchini kuruhusu askari wake kununua sare kwa watu binafsi. Askari wa jeshi hilo wameibuka na kudai kuwa wamekuwa wakiuziwa sare hizo kwa shilingi 45,000.

photo-8-1
Wakizungumza jana kwa nyakati tofauti, askari mbalimbali waliohojiwa na gazeti la Habari Leo licha ya kumpongeza Rais Magufuli kwa kulikemea suala hilo, walisema ni rahisi kushona kombati uraiani kwa kuwa vitambaa vinapatikana madukani, lakini kofia na mkanda ikichakaa askari analazimika kutoa pesa ili kupata mavazi hayo.
“Hizi kofia na mikanda inatolewa bohari ya jeshi, lakini kuupata huko mkanda au kofia lazima utoe rushwa kwa askari anayefanya kazi pale,” alisema mmoja wa askari aliyehojiwa na gazeti hili.
Wengi wa askari hao walisema kutokana na ugumu wa kupatikana na kofia na mikanda ya jeshi hilo, wengi wao wanaendelea kutumia kofia na mikanda waliyopewa wakati wanamaliza mafunzo.
Walisema kinachotolewa bure na jeshi hilo kwa sasa ni vyeo tu na sio sare nyingine yoyote. “Kofia hii ninayotumia pamoja na mkanda ni ile niliyopewa wakati namaliza depo (mafunzo) mwaka 2001,” alisema askari huyo ambaye ana miaka 15 sasa kazini na kuongeza, “Magereza wanachotoa bure kwa askari wao ni zile alama za cheo tu, vingine vyote vinavyohusu sare lazima askari ajinunulie.”
Wakati askari Magereza wanajinunulia sare, serikali imekuwa inatoa mamilioni ya fedha kwa ajili ya kuwahudumia askari hao. Mfano, katika bajeti ya mwaka 2015/16 serikali ilitoa Sh bilioni 167.1 kwa jeshi hilo.

Kati ya fedha hizo, Sh bilioni 67.7 zilitolewa kwa jeshi hilo kwa ajili ya matumizi mengineyo, Sh bilioni 97.7 kama mishahara na fedha za maendeleo zilizotolewa kwa polisi ni Sh bilioni 1.6 Askari mmoja ambaye yuko mkoani Simiyu aliyefanya mahojiano na gazeti hili, alisema upatikanaji wa sare za Magereza kwa askari walioko mikoani ni mbaya, kwani wamekuwa wanalazimika kununua suruali na shati kati ya Sh 40,000 na 45,00 na viatu Sh 40,000.

“Juzi nilikuja hapo Dar es Salaam, nikawa na shida ya mkanda na kofia, nililazimika kutoa Sh 30,000 ambayo kofia niliinunua kwa Sh 10,000 na mkanda nilinunua kwa Sh 20,000,” alisema askari huyo ambaye hakupenda jina lake liandikwe gazetini. Alipoulizwa anazipataje sare za jeshi hilo, alifafanua, “Sisi ukitaka sare unaenda kwa fundi unachukuliwa vipimo vya shati na suruali, unamtumia askari mwenzako wa Dar es Salaam anakununulia kitambaa na kukushonea, kisha anakutumia.”
Alisema yeye tangu amalize mafunzo mwaka 2009 hajawahi kupewa sare yoyote. “Sijawahi kupewa mkanda, kofia wala viatu vyote tunajinunulia… mkanda nilio nao na kofia ambayo imeisha nilipewa wakati namaliza mafunzo, hadi juzi nilipokuja huko ndipo nikafanya jitihada za kupata kofia na mkanda mwingine,” alisema
CHANZO:HABARI LEO

No comments:

Post a Comment