Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha ACT – Wazalendo na Vyama vingine vyenye wagombea wa Ubunge katika Uchaguzi Mdogo wa Jimbo la Dimani na Udiwani katika Kata Ishirini (20) za Tanzania Bara ,kuwasilisha malalamiko ya ukiukwaji wa Maadili ya Uchaguzi kwenye Kamati za Maadili zilizo katika maeneo yao.
Akizungumza na vyombo vya habari jana jijini Dar es salaam, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Bw. Kailima Ramadhan alisema NEC imepata taarifa kupitia Vyombo mbalimbali juu ya malalamiko ya Chama Cha ACT-Wazalendo kuvilalamikia Vyombo vya Dola pamoja na Watendaji wa Umma kufanya vitendo vyenye muelekeo wa kukipendelea Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Bw. Kailima alisema taarifa ya Chama hicho iliyotolewa kwenye Vyombo vya Habari Januari, 12 2017, imeeleza kuwa Watendaji wa Halmashauri ya Geita waliwakusanya Wazee katika Kata ya Nkoma waje na Vitambulisho vyao vya kupigia Kura kwa lengo la kuwapatia huduma ya afya bure jambo linalolalamikiwa na ACT- Wazalendo kwa madai kwamba Watendaji hao wana lengo la kuwahadaa Wazee hao ili wakipigie Kura Chama Cha Mapinduzi (CCM).
No comments:
Post a Comment