Thursday 19 January 2017

PICHA:Ukweli kuhusu Maiti iliyozikwa na Kisha Baadae Kukutwa Nyumbani Kitandani.

Maiti ya mtoto Haruna Kyando (9) ambayo ilikutwa nyumbani muda mfupi baada ya wananchi kutoka makaburini kumzika, imezikwa kwenye makaburi ya Isanga chini ya ulinzi wa askari wa Jeshi la Polisi nchini, huku waombolezaji wakiaga mwili huo kwa kufunuliwa jeneza eneo la kichwani makaburini hapo.

Aidha, Mchungaji wa Kanisa la Bonde la Baraka, ameingizwa lawamani kwa kupotosha umma.

Haruna aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kifafa tangu udogo wake, alikutwa na wazazi wake Jailo Kyando (36) ambaye ni muosha magari na mkewe, Anna Elieza (32) akiwa amefia usingizini Jumatatu wiki hii nyumbani kwao Mtaa wa Igoma A, Kata ya Isanga jijini Mbeya.

Kilichowapa taharuki wakazi wengi jijini hapa ni baada ya ndugu, jamaa na marafiki wa familia ya Haruna walipotoka makaburini siku hiyo walikokwenda kuzika, waliporejea nyumbani waliukuta mwili wa mtoto huyo ukiwa umelazwa kwenye godoro, pale pale ulipowekwa wakati walipokuwa wakiuandaa kuuweka kwenye jeneza.

Hatua hiyo ilizua taharuki kubwa kiasi cha wananchi kutaka kufahamu ni kitu gani kilichozikwa ndani ya jeneza na ndipo Jeshi la Polisi lilipoingilia kati, kuzuia kufukuliwa kwa kaburi husika.

Hatua hiyo ilisababisha vurugu na hatimaye saa tatu za usiku siku hiyo hiyo ya maziko ya awali, Polisi wakalazimika kutumia mabomu ya machozi, kutawanya watu waliofurika katika makaburi ya Isanga wakishinikiza kaburi lifukuliwe.
Nusu saa baadaye jeneza la mtoto huyo lilitolewa nje ya kaburi na ndipo Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma A, Fredy Mwaiswelo alipofunua jeneza na kukuta ndani kukiwa tupu, hali iliyoashiria mwili wa marehemu haukuwekwa ndani ya jeneza wakati wanakwenda kuzika.

Kutokana na hali hiyo, Polisi kwa kushirikiana na baadhi ya vijana, walibeba jeneza hilo na kuelekea nalo katika Kituo cha Polisi kwa ajili ya uchunguzi zaidi kabla ya kuwakabidhi tena wanandugu mwili ili kuendelea na taratibu za maziko kwa mara nyingine.

Jeneza baada ya kufukuliwa kutoka kaburini
Mwenyekiti wa Mtaa wa Igoma pamoja na Baba wa Marehemu wakifunua jeneza kuhakikisha kama kulikuwa na mwili wa marehemu 
Jeneza lililofukuliwa likiwa halina kitu ndani yake 
Vijana wakiwa wanaondoa jeneza makaburini na kulipeleka kituo cha Polisi kwa ajili ya taratibu zingine

No comments:

Post a Comment