Saturday, 18 February 2017

Ukweli wa Hans van Pluijm ya kuhusu hali ya Yanga Katika michuano ya kimataifa.

Image result for Hans van Der Pluijm
Yanga haijafanya mabadiliko makubwa katika kikosi chake na tayari imeanza mechi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa ushindi wa mabao 5-1, hivyo Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo, Hans van Der Pluijm amesema watafika mbali.

Pluijm ambaye ni raia wa Uholanzi ameliambia Championi Jumamosi kuwa, Yanga itafika mbali kwenye michuano hiyo ya Shirikisho la Soka Afrika (Caf) kutokana na mwenendo mzuri ambao wameanza nao msimu huu.

Leo Jumamosi Yanga inatarajiwa kurudiana na Ngaya Club de Mbe ya Comoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam baada ya awali kushinda mabao 5-1 huko Moroni, Comoro.

Pluijm ambaye amewahi kuifundisha timu ya Berekum Chelsea ya Ghana, alisema ana uhakika wa Yanga kufanya vizuri kwani ina kikosi kilichokaa pamoja kwa muda mrefu, hivyo wana nafasi nzuri ya kupata ushindi.

“Ni mwanzo mzuri ambao tumeanza nao na ushindi huo tulioupata utakuwa chachu kwetu ya kuendelea kupata matakeo mazuri kwenye michuano hiyo.
“Kama tukiendelea kufanya hivi katika kila mechi, basi tuna kila sababu ya kufika mbali kutokana na kikosi kipana tulichonacho, pia wachezaji hawa wamekaa pamoja muda mrefu.

“Wachezaji wengi wana uzoefu na michuano hii na hilo ndilo linalonipa zaidi msukumo wa kusema Yanga itafika mbali na utaamini maneno yangu baadaye,” alisema Pluijm.


Msimu uliopita, Yanga iliishia raundi ya tatu katika Ligi ya Mabingwa Afrika kisha ikatua katika Kombe la Shirikisho ambako iliishia hatua ya makundi.

No comments:

Post a Comment