Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, IGP Simon Nyakoro Sirro amefanya mabadiliko katika Jeshi la Polisi kwa kuwabadilisha baadhi ya viongozi wa jeshi hilo kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine huku wengine kupandishwa vyeo vyao.
Katika mabadiliko hayo, IGP Sirro amemteua Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) Juma Yusuf Ally kuwa Kaimu Kamishna wa Polisi Zanzibar.
Uteuzi huo unafuatia kustaafu kwa aliyekuwa kamishna wa Polisi Zanzibar Kamishna Hamdani Omari Makame kwa mujibu wa sheria baada ya kutimiza umri wa miaka sitini (60). Kabla ya uteuzi huo DCP Juma alikuwa ni Mkuu wa Utawala na Fedha Makao Makuu ya Polisi Zanzibar.
IGP Sirro pia amemteua Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Lazaro Mambosasa kuwa Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, kabla ya uteuzi huo SACP Mambosasa alikuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma.
Kufuatia uteuzi huo, aliyekuwa Kaimu Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam anakwenda kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, na aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Neema Mwalimu Mwanga anakwenda Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam.
IGP Sirro pia amemteua aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Temeke Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Gilles Bilabaye Mroto kuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma na Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Emmanuel Lukula kwenda kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Kipolisi Temeke. Kabla ya uteuzi huo, ACP Lukula alikuwa Afisa Mnadhimu wa Polisi mkoa wa Mbeya.
Kwa upande mwingine, Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi wote kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kufichua taarifa za uhalifu na wahalifu ili kwa pamoja ili waweze kuendelea kuiweka Tanzania salama.
No comments:
Post a Comment