Thursday, 24 August 2017

TFF Wafunguka kuhusu makosa ya Uandishi wa Ngao ya Jamii.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limeomba radhi wanafamilia wote wa mpira wa miguu nchini kutokana na makosa ya kiuandishi yaliyoonekana kwenye utambulisho wa Ngao ya Jamii iliyotolewa Jumatano Agosti 23, 2017 kwa klabu ya Simba.

Ngao hiyo ilitolewa mara baada ya mchezo uliokutanisha timu za Simba SC na Yanga SC zote za Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Katika mchezo huo, Simba ilishinda kwa mikwaju ya penalti 5-4 dhidi ya Yanga na kutwaa ngao hiyo.

Makosa yaliyoonekana katika ngao hiyo ya jamii ni kukosewa kuandikwa kwa neno “SHIELD” ambapo liliandikwa “SHEILD” na hivyo kupoteza maana yake ya msingi.

Katika taarifa ya TFF iliyotolewa leo Agosti 24 wamesema kwamba “Watanzania hususani wanafamilia ya mpira wa miguu popote pale, TFF hatujapokea vizuri mwonekana wenye makosa kwenye Ngao hiyo ya Jamii kama ambavyo wadau hawajapokea vema suala hili.”

Kuonyesha kukerwa na uzembe huo uliofanywa na baadhi ya viongozi wake, Kaimu Katibu Mkuu wa TFF, tayari amechukua hatua za kinidhamu kwa watumishi waliohusika.

Mbali na hilo, kiongozi huyo amewasiliana na uongozi wa Simba SC kuirejesha ngao hiyo ili kufanyiwa marekebisho yatakayobaki kwenye kumbukumbu sahihi. Uongozi wa TFF umesisitiza kuwa hatutegemei tukio kama hili kujirudia tena.


No comments:

Post a Comment