Klabu ya Mabingwa watetezi ligi kuu bara , Young Africans imewataka mashabiki wa timu hiyo kupuuza maneno ya chuki yanayoenezwa kuhusu timu yao huku ikiwaahidi kuwa timu ina wachezaji wazuri wenye uwezo wa kutetea ubingwa wao msimu huu.
Kupitia taarifa iliyotolewa kupitia mtandao wa klabu hiyo imesema kuwa timu yao imejipanga kuchukua ubingwa kwa mara ya nne mfululizo hivyo mashabiki wanapaswa kuwa na imani huku wakitakiwa kujitokeza uwanjani pindi timu hiyo inapokuwa ikisakata kabumbu.
Aidha taarifa hiyo imewatoa wasiwasi mashabiki wa timu hiyo kwa kusema kuwa wachezaji ambao waliokuwa majeruhi, afya zao zinaendelea vizuri na inawezekana katika mchezo ujao wakawepo uwanjani.
"Wachezaji wetu majeruhi wanaendelea vizuri na ninauhakika mkubwa sana Chira, Mwashiuya, Tambwe na Benno katika mchezo ujao watakuwepo uwanjani huku suala la Pius Buswita likiwa linashughulikiwa kwa uzuri zaidi na karibuni suluhisho litapatikana", Sehemu ya taarifa hiyo ilisema.
Hata hivyo klabu hiyo imewashukuru mashabiki wote waliojitokeza uwanjani katika michezo iliyopita huku ikisisitiza ushirikiano uendelee haswa katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa na Njombe Septemba 06 katika uwanja wa sabasaba mjini Njombe.
No comments:
Post a Comment