Wanachama 13 wa Chama Cha Wananchi (CUF) kinachoongozwa na Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na msajili wa Vyama Vya Siasa Profesa Lipumba wametoka nduki mahakamani baada ya kesi yao kufutwa.
Watuhumiwa hao 13 wamekimbia ndani ya Mahakama wakihofia kukamatwa tena baada ya hakimu kuondoa kesi yao mahakamani hapo leo, Wakili wa watuhumiwa hao Bw. Hashimu Bakari amesema kuwa kesi inapofutwa ina maana kuwa mtuhumiwa hana hatia yoyote na anatakiwa kuondoka na kurudi zake nyumbani.
"Ndani ya miezi sita iliyopita kila tukija mahakamani kwa kila mwezi upande wa Jamhuri na upande wa DPP wanasema upelelezi umekamilika wanakuja na hoja za awali lakini hoja hazisomwi kwa hiyo mahakama tukufu 225 kifungu kidogo cha kwanza na vifungu vinavyofuata kuifuta kesi kwa sababu kesi inatakiwa kuanza kusikilizwa baada ya siku sitini tangu upelelezi kukamilika lakini hii kesi ilianza toka mwezi wa 11, mwaka 2016 mpaka leo haijaendelea sasa kesi imefutwa" alisema Wakili Hashimu
Aidha Wakili huyo anasema kesi kufutwa tafsiri yake ni kwamba watu wako huru na wanaweza kwenda nyumbani
"Kwa nchi za kidemokrasia tafsiri ya kesi kufutwa maana yake ni kwamba mshtakiwa hana kosa yupo huru anatakiwa kurudi nyumbani kuendelea na mambo mengine ya ujenzi wa taifa, kama kuna utaratibu mwingine wa Jamhuri kumkamata mtuhimiwa unafuata kama ilivyokuwa katika kesi ya awali " alisema Wakili Hashimu
Wafuasi hao wa CUF wameachiwa na Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa chini ya kifungu cha 225 cha Sheria ya Makosa ya Jinai lakini kifungu hicho kinaruhusu upande wa mashtaka kuwakamata tena washtakiwa pale wanapoona inafaa, watuhumiwa hao waliona wakimbie kuepuka kukamatwa tena jambo ambalo baadhi ya polisi na magereza walionekana kuwadhibiti watuhumiwa hao ili waweze kuwakamata tena.
No comments:
Post a Comment