Ukisema Neymar hakamatiki Ufaransa wala hautakuwa umekosea, kwani anaonekana anataka kuwa mfalme mpya baada ya kufunga mabao mawili wakati PSG ikiitwanga Toulouse kwa kwa mabao 6-3.
Maana yake ndani ya mechi mbili, Neymar aliyesajiliwa kwa dau kubwa zaidi la usajili la pauni milioni 198 kutoka Barcelona, tayari amepachika mabao matatu kwa kuwa mechi ya kwanza alifunga bao moja.
Neymar alikuwa wa kwanza kufunga kwa PSG katika dakika ya 31, akiisawazishia baada ya Toulouse kutangulia katika dakika ya 18 kwa bao la Max-Alaon Gradel.
Adrien Rabiot akapokea pasi ya Neymar katika dakika ya 35 na kuifungia PSG bao la pili na mapumziko ikawa 2-1.
Kipindi cha pili, katika dakika ya 69, PSG ilipata pengo baada ya kiungo wake Marco Veratti kutolewa kwa kadi nyekundu baada ya kulambwa kadi ya pili ya njano.
Edinson Cavani aliandika bao la tatu dakika ya 75 kwa mkwaju wa penalti lakini Toulouse wakakomaa na kupata bao la pili dakika ya 78 mfungaji akiwa Christopher Jullien.
Angel Di Maria akafanya yake na kutoa pasi kwa Javier Pastore aliyefunga bao ;a nne dakika ya 82 na dakika mbili baadaye, Neymar akampa pasi safi Layvin Kurzawa aliyeandika bao la tano.
Wakati ikionekana kama “imetosha”, Neymar alifunga bao la sita katika dakika 90 likiwa ni la pili kwake katika mechi hiyo la la tatu katika mechi yake ya pili ya League 1.
No comments:
Post a Comment