Saturday, 5 August 2017

Yanga kumshitaki Dewji kwa kuvujisha jezi.

Image result for Kassim Dewji
Uongozi wa Yanga umepanga kumshitaki Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Kasim Dewji kwa kudaiwa kuvujisha jezi za timu hiyo.

Yanga inamshutumu Dewji kwa kuipatia jezi Kampuni ya Huduma za Simu ya Vodacom Tanzania ambayo ilizitambulisha juzi katika hafla ya kukabidhi vifaa vya michezo kwa timu za Ligi Kuu Bara kwa ajili ya msimu ujao wa ligi hiyo.

Katika hafla hiyo ya kukabidhi vifaa vya michezo kutoka kwa Vodacom ambao ni wadhamini wa ligi hiyo, Yanga haikuwakilishwa na kiongozi yeyote yule.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Yanga, Salum Mkemi alisema jezi hizo zilizotambulishwa na Vodacom katika hafla hiyo kuwa wameinunulia timu hiyo kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu ni uongo.

Alisema Vodacom haijawanunulia jezi hizo bali jezi hizo ni mali yao walizonunuliwa na wadhamini wao wakuu Kampuni ya SportPesa kwa ajili ya kuiwezesha klabu hiyo kujipatia fedha kwa kuziuza.

Yanga ilizipeleka jezi hizo kwa Dewji ambaye ni wakala wa kuuza jezi nchini kwa ajili ya kubandikwa nembo ya klabu hiyo pamoja na kuandikwa maandishi ya wadhamini wao.

“Tumeshangaa sana kuona jezi zetu hizo zinatambulishwa Vodacom wakati sisi tulikuwa bado hatujazitambulisha kwa sababu tulitaka zitambulishwe na mchezaji wa zamani wa Arsenal, Sol Campbell ambaye analetwa na SportPesa.

“Dewji ametuvurugia mipango yetu kwa hiyo hivi sasa tunajipanga ili kuona ni hatua gani tutazichukua na ikiwezekana kumshitaki Dewji kutokana na kitendo chake hicho cha kutuhujumu,” alisema Mkemi.

Hata hivyo, alipotafutwa Dewji ili aweze kulizungumzia suala hilo, hakupatikana kutokana na simu yake ya mkononi kuita bila ya kupokelewa.

No comments:

Post a Comment