Kocha msaidizi wa Simba Mganda Jackson Mayanja amekanusha taarifa za kutimuliwa ambazo zinasambaa nchini na kudai kuwa si za kweli kwani hana taarifa yoyote rasmi kutoka kwa uongozi.
Mayanja amesema hajui taarifa hizo zinatoka wapi kwasababu sio za kweli na yeye anaendelea na kazi kama kawaida. “Sijafukuzwa naendelea na kazi yangu kama kawaida”, amesema Mayanja.
Aidha Mayanja amesema hakuwepo nchini kwa siku kadhaa zilizopita kwasababu alisafiri kwenda kwao Uganda ambako alikuwa na mambo ya kifamilia na tayari ameshayamaliza na amerejea kuendelea na kazi.
“Nilienda nyumbani Uganda mara moja kulikuwa na matatizo ya kifamilia sio kwamba nimefukuzwa, ndio mana nimerejea kuendelea na kazi yangu na uongozi wa klabu haujanipa taarifa yoyote, sasa sijui hizo taarifa zimetoka wapi”, ameongeza Mayanja.
Hivi karibuni kumekuwa na tetesi kwamba klabu ya Simba inataka kubadili benchi lake la ufundi lakini jana kupitia mkutano na wanahabari, afisa habari wa Simba Haji Manara alikanusha taarifa hizo na kudai kuwa klabu inaendelea na makocha wake Joseph Omog na Jackson Mayanja.
No comments:
Post a Comment