Rais wa Jamhuri ya Msumbiji Mhe. Filipe Jacinto Nyusi amefanya ziara ya kikazi ya siku moja hapa nchini ambapo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli Mjini Dodoma.
Mhe. Filipe Jacinto Nyusi amepokelewa katika uwanja wa ndege wa Dodoma na mwenyeji wake Mhe. Rais Magufuli aliyeongozana na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na kisha viongozi hao wamefanya mazungumzo rasmi na kusalimu wananchi kupitia vyombo vya habari.
Mhe. Rais Nyusi amemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kumpokea na kufanya nae mazungumzo na amesema ujio wake umelenga kuimarisha na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wa kihistoria na kidugu kati ya nchi yake na Tanzania.
“Mhe. Rais Magufuli japo kuwa nimetoa taarifa ya muda mfupi kuwa nakuja kuonana nawe, umenikaribisha umenipokea na tumezungumza mambo yenye manufaa kwa nchi zetu, nakushukuru sana” amesema Mhe. Rais Nyusi.
Amebainisha kuwa yeye na Rais Magufuli wamezungumzia namna Tanzania na Msumbiji zitakavyobadilishana uzoefu kuhusu ugunduzi mkubwa wa gesi na mafuta uliofanikiwa katika nchi hizi, masuala ya ulinzi na usalama na uimarishaji wa miundombinu ya usafiri.
Kwa upande wake Mhe. Rais Magufuli amemshukuru Mhe. Rais Nyusi kwa kuja Mjini Dodoma na kwa kudumisha uhusiano na ushirikiano wa kidugu na kihistoria uliojengwa na waasisi wa mataifa haya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Samora Machel wa Msumbiji.
Mhe. Rais Magufuli amesema katika mazungumzo hayo pia wamekubaliana Tume ya pamoja ya ushirikiano ya Tanzania na Msumbiji zikutane haraka ili kuimarisha maeneo yote ya ushirikiano kwa manufaa ya nchi hizo.
“Nafurahi kuwa Mhe. Rais Nyusi pia amesema Msumbiji itatoa kibali kwa Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) kufanya safari za moja kwa moja kati ya Tanzania na Msumbiji haraka iwezekanavyo, ili kurahisisha usafiri kati yetu” amesisitiza Mhe. Rais Magufuli.
Mhe. Rais Nyusi ameondoka nchini jana jioni na kurejea nchini Msumbiji.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dodoma
No comments:
Post a Comment