Ofisa Habari Msaidizi wa TFF Clifford Ndimbo |
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limemha-lalisha straika wa Yohana Nkomola kuvaa uzi wa Yanga na ataanza kupiga mzigo kesho Jumapili dhidi ya timu ngumu ya Mbao FC jijini Mwanza.
Mchezaji huyo aliyewahi kufanya majaribio nchini Tunisia, ni miongoni mwa wachezaji waliosajiliwa katika usajili wa dirisha dogo kupewa leseni baada ya mfumo wa usajili wa kielektroniki wa Fifa-TMS kukaa sawa.
Awali, Nkomola na wachezaji wengine walizuiliwa kucheza mechi za Ligi Kuu Bara na zile za Kombe la FA ambayo Yanga iliifunga Reha FC mabao 2-0 kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam.
Hii ina maana kwamba, Yanga kesho Jumapili itakuwa na nafasi ya kumtumia Nkomola ambaye ni mchezaji wa timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys iliyoshiriki Afcon ya Gabon.
Ofisa Habari Msaidizi wa TFF, Clifford Ndimbo alisema leseni hizo zimetolewa jana Ijumaa kwa klabu ikimaanisha ni ruksa kuwatumia wachezaji ambao wamewasajili katika dirisha dogo.
Ndimbo alisema leseni hizo zilichelewa kutoka kutokana na TMS kusumbua, hivyo tayari wamezitaarifu klabu zote kuwa ni ruksa kuwatumia wachezaji wapya kuanzia mechi za jana Ijumaa na wikiendi hii.
“Kilichochelewesha leseni hizo ni matatizo ya mtandao wa Fifa ambao hivi sasa umekaa vizuri, hivyo wachezaji wote waliosajiliwa dirisha dogo watumike,” alisema Ndimbo ambaye kitaaluma ni Mwanahabari.
Kutokana na kuchelewa kutoka kwa leseni hizo, wachezaji wengi waliosajiliwa wakati wa usajili wa dirisha dogo hawakuweza kuzichezea timu zao katika mechi za Kombe la FA.
No comments:
Post a Comment