Tuesday, 30 January 2018

Kiasi cha pesa iliyopata Serikal baada ya kuuza Meno ya Viboko.

Image result for HIPPO
Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa  Wanyamapori Tanzania (TAWA)  imefanya mnada wa hadhara wa kuuza meno ya viboko vipande  12,467 yenye uzito wa kilo 3,580.29   katika   ofisi  zake ndogo katika  Jengo la Mpingo,  jijini Dar es Salaam ambapo jumla ya makampuni  19 yenye leseni daraja la kwanza yameshiriki  katika mnada huo.

Mnada huo umefanyika  chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha na Mipango ambapo  kampuni ya  On Tours Tanzania Limited  imeibuka mshindi kwa kwa kununua meno hayo kwa jumla ya shilingi  30,900,000/=


Awali akizungumza katika mnada huo, Mwenyekiti kutoka Wizara ya Fedha na Mipango, Karerema Kwaleh aliwataka wafanyabiashara kuzingatia masharti mnada huo.

Ambapo Karerema alimtaka mfanyabiashara yeyote  atakeibuka mshindi  kulipia asilimia ishirini na tano (25%) ya bei papo hapo na asilimia sabini na tano (75%) italipwa yote katika muda wa siku kumi na nne (14) baada ya mnada.

Kufuatia sharti hilo baada ya kutangazwa kwa  mshindi,  Mwakilishi  kutoka Kampuni hiyo, Grey Kilas   aliweza  kulipia asilimia kiasi hicho cha  asilimia ishirini na tano (25%) papo hapo na asilimia sabini na tano (75%) atailipia  ifikapo  Februari 11, 2018.

Wakati huohuo,  Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu TAWA, Mabula Misungwi  amewatoa wasiwasi wananchi kuwa biashara  hiyo haiwezi  kuchochea ujangili kwa vile meno hayo  yanauzwa kwa  wafanyabiashara  wale tu wenye  leseni za nyara daraja la kwanza

Mabula amesema meno hayo yalianza  kukusanywa tangu mwaka 2004 na huko nyuma serikali ilikuwa ikiyauzia makampuni yenye leseni lakini kwa mwaka huo wameanza utaratibu mpya wa kuuza meno hayo kwa njia ya mnada.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Kampuni hiyo, Grey Kilas ameishukuru wasimamizi wa mnada huo kuwa umeendeshwa kwa uwazi wa hali ya juu na umetoa fursa kwa kila mmoja wao

Akizungumzia kuhusu soko, Kilasi  amesema meno hayo  huuzwa nchini  Japan, Marekani na Hongkong ambapo hutumika katika kutengenezea mapambo kama vile stempu pamoja na vishikizo vya nguo.

Itakumbukwa kuwa kwa mara mwisho  biashara hiyo ya kuuza meno ya viboko ilifanyika mwaka 2004.

No comments:

Post a Comment