Kocha Msaidizi wa Simba Mrundi, Masoud Djuma amesema nguvu zao wamezielekeza kwenye mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Al Masry ya Misri na baada ya hapo wanarejea kwenye Ligi Kuu Bara kupambana na Yanga.
Kauli hiyo ameitoa kocha huyo baada ya Yanga kuwafikia kwa pointi 46 katika msimamo wa ligi huku Simba wakiongoza kwa idadi ya mabao ya kufunga ambayo ni 49 huku watani wao wakiwa na 38.
Simba leo inatarajiwa kusafiri kwenda Misri kuwafuata Al Masry watakaovaana Jumamosi hii kwenye Uwanja wa Port Said unaoingiza mashabiki 17,988.
Djuma alisema hivi karibuni walikutana na kufanya kikao na wachezaji wao na kikubwa waliwasisitiza kusahau matokeo ya watani wao Yanga katika ligi na badala yake kuelekeza akili zao mchezo dhidi ya Al Masry.
“Katika kuhakikisha tunapata matokeo mazuri mechi na Al Masry, tumeona kukutana na wachezaji wetu na kikubwa ni kuwatengeneza kisaikolojia kwa lengo la kusahau matokeo ya Yanga wanayoendelea kuyapata katika ligi.
“Tukiingiza matokeo ya Yanga wanayoendelea kuyapata yatawafanya wachezaji wetu washindwe kucheza na kuifikiria ligi kuu, kitu hatutaki kiwatokee wachezaji wetu na tayari tumeanza kulifanyia kazi kwa kukaa na wachezaji wetu.
“Tumewaambia kuwa, tumalize mchezo wetu wa marudiano na Al Masry kwanza na baada ya hapo tutarudi kwenye ligi na kikubwa ni kuendelea kupata matokeo mazuri ili tuongoze katika msimamo na ikiwezekana kushinda mechi zetu zote,” alisema Djuma.
No comments:
Post a Comment