Friday 27 November 2015

Elimu ya Tanzania na maajabu yake

 


Maamuzi na miongozi mbalimbali inayotolewa kuhusu elimu, imekuwa ikiwashangaza wadau wa elimu na jamii kwa jumla.
Hivi karibuni, Serikali kupitia Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta), ilitangaza kuwa wanafunzi watakaofeli mtihani wa darasa la nne na kidato cha pili hawatarudia darasa, badala yake wataandaliwa utaratibu maalumu wa masomo ya jioni.
 “Lengo la kuweka utaratibu huo ni kusimamia kwa karibu viwango vya ufundishaji. Wanafunzi wanaofanya vibaya wanahitaji ukaribu wa walimu na siyo kuwarudisha darasa tu,” anasema Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde.
Akiupokea uamuzi huo, Katibu Mtendaji wa Umoja wa Wamiliki wa Shule na Vyuo nchini (Tamongsco), Benjamin Nkonya, alisema: “Huu ni msumari wa mwisho kwenye jeneza la elimu. Serikali ikizuia wanafunzi kurudia darasa, elimu itaporomoka kama ilivyokuwa miaka 40 iliyopita na shule za binafsi zitakua kwa kasi

Hii siyo mara ya kwanza kwa Serikali Tanzania kutoa maagizo yanayoashiria kuifanyia istihzai sekta ya elimu, historia inaonyesha kuwapo kwa matukio mengi ya viongozi wa Serikali na wanasiasa kuichezea sekta hiyo; tuangalie mifano kadhaa.
Kufutwa masomo ya kilimo
Katika nchi inayojinasibu kuwa ya kilimo kwa kudai kuwa sekta hiyo ndiyo uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa, ingetarajiwa kuwa na mifumo thabiti ya utoaji wa elimu ya kilimo, hali haikuwa hivyo.
Aliyekuwa Waziri wa Elimu na Utamaduni katika Serikali ya awamu ya tatu, Joseph Mungai, alifuta masomo ya kilimo. Si kilimo pekee, waziri huyo pia alifuta michezo akidai kuwa iliwakosesha walimu na wanafunzi muda wa kufundisha na kujifunza.
Masomo ya sayansi yachanganywa
Kioja kingine kilichofanywa uongozi wa Mungai ulikuwa agizo lake la kuchanganywa kwa masomo ya Kemia na Fizikia na kuwa somo moja, kwa hoja kuwa silabasi ya sekondari ilikuwa na masomo mengi hali iliyochangia ugumu wa ufundishaji wa masomo ya sayansi, lugha na Hisabati.
‘’Tulijitahidi kupunguza wingi wa masomo na kuongeza vipindi vya lugha na hisabati view kila siku… Kitaaluma unaweza kusoma somo la sayansi ndani yake zikiwamo mada za Biolojia, Kemia na Fizikia... alisema Mungai alijitetea Mungai alipohojiwa na gazeti hili Machi 16, 2013.
Ujenzi wa shule za kata
Pamoja na haja na umuhimu wake, ujenzi wa shule hizo ni sehemu ya maajabu ya kielimu kwa sababu uamuzi wa kuzijenga ulifanywa kwa pupa pasina kuwapo kwa maandalizi thabiti ya miundombinu, vifaa na walimu.
Uko ushahidi miaka ya mwanzo ya utawala wa awamu ya nne, baadhi ya shule za kata zilianza zikiwa na darasa moja au mawili; nyingine mpaka leo zina walimu wasiokidhi haja. Kwa mfano, vyombo vya habari vimewahi kuripoti mara kadhaa kuwapo kwa shule zenye wanafunzi zaidi ya 200 lakini zina mwalimu mmoja au wawili.
Shule nyingi za kata hazina vyumba vya maktaba wala maabara. Ni mpaka mwishoni mwa ngwe ya pili ya awamu ya nne, Serikali ikatoa amri kila shule ya kata kujenga maabara, mchakato ambao hadi makala haya yanachapishwa unaendelea japo kwa kasi isiyoridhisha.
Kuajiri walimu wasio na sifa
Baada ya hamasa kubwa ya uongozi wa awamu ya nne kutaka kujengwa kwa shule za sekondari kwa kila kata, shule hizo zilijikuta hazina walimu.
Kutatua tatizo hilo, Serikali iliwashangaza wadau wa elimu na wapenda maendeleo nchini kwa kuruhusu utolewaji wa mafunzo ya muda mfupi kwa walimu. Walimu hawa waliomaliza kidato cha sita maarufu kwa jina la utani la Voda fasta walifundishwa kwa muda wa wiki sita na kisha kupewa leseni ya kufundisha. Kwa kawaida walimu wa cheti na diploma husomea miaka miwili na wa shahada kati ya miaka mitatu na minne
Kufutwa mtihani wa kidato cha pili
Mwaka 2008, Serikali ilipunguza makali ya mtihani wa mchujo kwa wanafunzi wa darasa la nne na wa kidato cha pili iliposema “mitihani ya ngazi hiyo isiwe kikwazo cha maendeleo ya elimu.” Kauli hiyo ya aliyekuwa rais, Jakaya Kikwete ilichukuliwa kama agizo kwamba wanafunzi waliofeli waruhusiwe kuendelea na masomo ya darasa la tano hadi la saba na kidato cha tatu hadi cha nne.
Moja ya athari za kufutwa kwa mitihani hii ni kuwajengea au kuhamasisha uvivu wa kujifunza miongoni wa wanafunzi, kwani walibweteka wakiamini kuwa hakukuwa na kikwazo cha kuwazuia kufanya mtihani wa darasa la saba na wa kidato cha nne.
Ndiyo maana wakati uamuzi huo ukifanya kazi, miaka michache baadaye, Taifa lilishuhudia idadi kubwa ya wanafunzi waliofeli mitihani ya mwisho, kwa kuwa hapakuwa na utaratibu wowote wa kuwachuja katika madarasa ya chini.
Mbumbumbu wachaguliwa sekondari
Kama kuna vioja ambayo havitosahaulika katika historia ya nchi hii ni pamoja na kuwapo kwa taarifa za wanafunzi wasiojua kusoma na kuandika kuchaguliwa kuingia kidato cha kwanza.
Aprili 2012, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, ilibaini wanafunzi 5,200 waliojiunga sekondari walikuwa hawajui kusoma wala kuandika.
Kwa mfumo wetu wa elimu nchini, si ajabu kuona baadhi ya wahitimu wakimaliza elimu ya msingi bila ya kuwa na stadi hizo muhimu maishani, lakini kilichowashangaza wengi ni taarifa kuwa wanafunzi hao walichaguliwa na vyombo vya Serikali kuendelea na masomo ya sekondari.
Tukio hili liliacha maswali mengi kwa wadau wa elimu na jamii kwa jumla. Ni hatua iliyodhihirisha kuwapo kwa udhaifu mkubwa wa kiutendaji katika vyombo vinavyosimamia elimu.
Pia, hatua hiyo iliwaaminisha baadhi ya watu kuwa pengine kuna mchezo uliofanywa kwa makusudi wa kufaulisha wanafunzi hata wasio na sifa, kwa minajili ya kupendezesha takwimu za ongezeko la wanafunzi.
Ikumbukwe kuwa mara kwa mara, viongozi wanapojinadi kwa mafanikio katika sekta ya elimu, jambo kubwa wanalojinasibu nalo ni ongezeko la usajili wa wanafunzi katika madaraja mbalimbali ya elimu.
Mabadiliko alama za ufaulu
Serikali ya awamu ya nne iliwahi kutoa uamuzi uliowaacha watu wengi midomo wazi. Huo ni uamuzi wa kupunguza alama za ufaulu kwa wanafunzi wa kidato cha nne, huku ikiua daraja sifuri na kubuni kile Serikali ilichokiita daraja la tano. Baada ya wananchi kulalamikia wamekuja na mfumo wa ukokotoaji kwa kutumia GPA.
Kwa kuwa imekuwa kama ada kwa mfumo wa elimu kuyumbishwa, pengine wadau wa na jamii kwa jumla wanasubiri kioja kitakachofuata baada ya uamuzi wa sasa wa kutaka wanaofeli kidato cha pili kuendelea na masomo ya kidato cha tatu

Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment