Friday, 27 November 2015

Mambo usiyojua kuhusu ziara ya Papa Francis nchini Kenya

Rais Uhuru Kenyatta akimweleza jambo Papa

Nairobi, Kenya.
 Kiongozi wa Katoliki duniani, Papa Francis ni kiongozi wa kwanza wa kanisa hilo kutoka mataifa ya Amerika aliyeko ziarani barani Afrika.
Kiongozi huyo anayetajwa kuwa na unyenyekevu mkubwa, jana aliendesha ibada maalumu mjini Nairobi na kutoa wito wa kukabiliana na makundi yenye kufuata siasa kali akisisitiza suala la umoja kuwa ndiyo nguzo maalumu ya kuushinda ugaidi duniani.
Katika mahubiri yake, Papa Francis amewaambia  viongozi wa  Kikristo na Kiislamu wa Kenya  kwamba hawana chaguo lingine isipokuwa kujadiliana juu ya kujilinda dhidi ya  mashambulizi ya kinyama ya Waislamu wenye itikadi kali yaliyoikumba nchi hiyo.
Kiongozi huyo alizaliwa katika mji wa Buenos Aires nchini Argentina Desemba 17, mwaka 1936 na kupewa jina la Jorge Mario Bergoglio. Baba yake, Mario, alikuwa mhasibu katika shirika la reli nchini humo. Mamake, Regina Sivori mama wa nyumbani aliyeshughulisha zaidi na kuwalea watoto wake watano.
Katika maisha yake ya ujana, Papa Francis alipenda sana kandanda na aliwahi kufanya kazi za kawaida kama kuwa mlinzi katika jumba la starehe. Katika shughuli zake za kidini kuna wakati viongozi wa kisiasa wa Argentina walimtaja kama mpinzani wao wa kisiasa.
Papa Francis anajiita mtu wa kawaida, msemo wake maarufu na ambao ameutumia mara kadhaa ni kwamba, “watu wangu ni maskini na mimi ni mmoja wao”. Kiongozi huyo anayeongoza zaidi ya waumini bilioni 1. 4 duniani, anatajwa maisha ya kawaida na katika nyumba ya kawaida iliyopo makao makuu ya Vatican. Kuna ripoti pia wakati mwingine huwa anajipikia mwenyewe chakula chake.
Hapendi mavazi ya kifahari
Hii ni kutokana na kwamba yeye ni wa huduma ya Wa-Jesuit. Wafuasi wa huduma hii ni makasisi waliojitolea kuishi maisha ya umaskini na kuwahudumia zaidi maskini na wasiojiweza miongoni mwa jamii. Kabla ya kuingilia shughuli za kidini na hatimaye kujiunga na chuo cha mafunzo ya kidini, aliwahi kufanya kazi katika maabara na pia kama mlinzi katika jumba moja la starehe huko Argentina. Badaye akiwa na umri wa miaka 33 alitawazwa kuwa kasisi wa Kanisa KatolikiHatimaye alipanda na kuwa Askofu wa Jimbo la Buenos Aires mwaka 1998 na miaka mitatu baadaye Papa John Paul II alimtawaza kuwa Kardinali.
Wanasiasa walimwita ‘mpinzani’
Alipokuwa Kardinali Serikali za Rais Néstor Kirchner na mrithi wake, Cristina Fernández de Kirchner zilimuona kiongozi huyo wa kidini kama mpinzani wao kisiasa.
Tangu enzi hizo hadi sasa Papa Francis msimamo wake ni kwamba “Ukimfuata Kristo lazima ufahamu kuwa kuwanyanyasa watu au kuwanyima haki zao ni dhambi kubwa sana.”
Viongozi kadhaa wa dini na madhehebu mengine wamemtaja Papa Francis kama kiongozi mwenye kupenda uhusiano bora miongoni mwa dini na madhehebu tofauti. Kwa mfano mwezi Novemba mwaka 2012 katika Kanisa Kuu la Kikatoliki mjini Buenos Aires, Papa Francis aliwaleta pamoja viongozi wa Kiyahudi, Waislamu na madhehebu ya kiuinjilisti katika ibada maalum ya pamoja ya kuombea amani na suluhu ya machafuko Mashariki ya Kati.

Chanzo:Mwananchi

No comments:

Post a Comment