Friday, 27 November 2015

SAIKOLOJIA: Unaweza kufanya watu wakuthamini?

Je unathaminiwa na watu katika jamii? Kama unathaminiwa ni mambo gani yanayokufanya uone kuwa unathaminiwa na kuhisi hivyo?
Moja katika mahitaji muhimu ya binadamu baada ya chakula, mavazi na malazi ni kuheshimiwa na kuthaminiwa na jamii. Binadamu ni kiumbe pekee aliye na daraja kuliko viumbe wengine wote duniani.
Kinachompandisha hadhi kuliko viumbe wengine ni uwezo wake wa kufikiri, ambao umemwezesha kuyatawala mazingira yake na kuyatumia ili kuboresha maisha yake.
Maendeleo na maisha yetu kwa jumla yanawategemea watu. Tunachokihitaji kutoka kwao ni kututhamini, kutujali na kutupenda.
Watu watatuthamini kutokana na matendo yetu na jinsi tunavyoonekana kwao. Hii ni kwa sababu imethibitishwa kuwa watu wenye muonekano wa hali ya juu mara nyingi huwa ndiyo mwenye mafanikio katika maisha.
Licha ya muonekano wetu kufanya tuthaminiwe na watu, unadhifu pia huwa na uhusiano na fikra zetu. Ndio maana viongozi wa dini, mashehe, mapadri, makasisi na wachungaji huvaa mavazi maalumu ambayo huwafanya wapate hisia fulani za mamlaka katika nafsi zao. Inasemwa kuwa askari hufikiri na kutenda kama askari anapokuwa anavaa sare za jeshi.
Niliwahi kusikia kisa cha ofisa na dereva wake  waliokwenda kwenye sherehe.
Walipofika waliegesha gari mbali na ukumbi. Hivyo watu hawakuwaona jinsi walivyokaa kwenye gari. Kwenye ukumbi kulikuwa na msichana aliyeandaliwa kumvisha mgeni shada la maua.
Ofisa na dereva walipofika mlangoni yule msichana alikwenda kumvisha shada la maua dereva huyo badala ya bosi wake huku watu wakimshangilia  kutokana na jinsi alivyoonekana nadhifu.
Dereva alikuwa  amependeza na kuonekana na hadhi kuliko bosi huyo.
Kwa hakika siyo sahihi kumthamini mtu kwa mavazi na muonekano wake pekee kwa sababu kuna mambo mengine muhimu kama vile akili, ujuzi na tabia. Lakini,  pia tukumbuke kuwa siku zote watu  hutupangia  thamani kutokana na jinsi tunavyoonekana kwao hasa wanapotuona kwa mara ya kwanza.
 Muonekano ndicho kitu cha kwanza ambacho hudumu zaidi katika fikra za mtu anayetuona kwa mara ya kwanza.
Aidha  muonekano huo huwa na taathira hata katika sifa zetu nyingine ambazo mtu huweza kuzigundua baada ya kutuona mara ya kwanza..
Mara ngapi tumewahi kuwasikia watu wakisema “Mtu kama yule hawezi kutenda jambo la kijinga kama hili” kipimo wanachokitumia hapa huwa siyo kingine isipokuwa anavyoonekana.
Je umewahi kuchunguza ni watu wa aina gani ambao huonekana wanaheshimika sana kwenya mkusanyiko wa watu kama vile  kituo cha basi,  sokoni au mkutanoni.
Utagundua kuwa wanaoheshimika zaidi ni wale walio nadhifu. Kwa kawaida watu huamini kuwa mtu aliye nadhifu ni wa maana, mwenye akili, msomi, kuaminika na kufanikiwa katika maisha. Mtu  anayeonekana mchafu watu humchukulia kama siyo mtu wa maana,  mwerevu, makini na hajendelea kimaisha.
Lakini mtu mwingine anaweza kukata tamaa kuwa hawezi kuonekana  nadhifu kwa kuwa hana fedha za kuweza kununulia mavazi ya thamani.
Hata hivyo, ikumbukwe kuwa ili mtu aonekane nadhifu siyo lazima avae nguo ghali.
Unadhifu ni kuvaa nguo safi na kuutunza mwili mzima katika hali ya usafi.
 Hakika ili tuwe nadhifu tunahitaji nguo nyingi zitakazotuwezesha kuwa katika hali hiyo kila siku.
Tukinunua nguo za bei nafuu tunaweza kupata nyingi na kuonekana nadhifu siku zote.
Hatuna budi kukumbuka kuwa unadhifu haushii tu katika manufaa ya kuwavutia  watu wanaokutazama bali hata kwako mwenyewe. 
Kadri  unanavyojighulisha  kujiweka  katika hali  ya unadhifu ndivyo kadri  unavyojijengea hali  ya kujithamini mwenyewe. Unapojithamini   ndipo na watu  wengine wanapokuthamini.
Kwa hakika unapojifikiria kuwa wewe ni duni na mtu  wa hali  ya  chini utaonekana vivyo hivyo kwa watu na utajipunguzia nafasi ya kuthaminiwa.
Kulikuwa na kijana mmoja ambaye hakusoma shule,  lakini hakupenda  kabisa watu wajue  hakusoma.
Hivyo  alikuwa  akijiweka  katika hali ya unadhifu wa hali ya juu siku zote. Alikuwa akiweka  kalamu mbili  hadi tatu  kwenye mfuko wa shati  lake.
Alipotembea  katika  mkono  mmoja  alishika gazeti  na mwingine  alibeba  mkoba. Siku moja aliingia Posta kumsalimu  rafiki yake  anayefanya  kazi  hapo.
Alipoingia  tu alikutana  na mzee mmoja  kutoka  mtaani  kwao  aliyemuomba  amjazie fomu.
Kijana aliona huo ni mtihani mkubwa  ambao  ungefichua  siri  yake.  Lakini alifikiri  haraka akaweza  kuvuka  mtihani  huo na kumwambia  mzee ana  haraka  sana, kisha akachukua  kalamu moja  katika mfuko wa shati  akampatia  mzee na  kumuomba  atafute mtu amjazie  fomu yake.
Kila ninapoikumbuka hadithi hii huzidi kuamini  kuwa  mtu anaweza kujitengenezea  mwenyewe  hadhi anayoipenda  na kuwafanya watu  wamthamini. Hata hivyo, pamoja  na kuwa nadhifu bado  kuna mambo  mengine ambayo mtu  anapaswa  kufanya  ili watu wa kuthamini kikamilifu. Watu  wanakuthamini sana  iwapo utaishi nao kwa  maelewano,  ushirikiano,  staha na adabu. Huna budi  kuwatendea  matendo  mema na kuwa  mwaminifu  na  mvumilivu.
Uepuke  maneno  ya  karaha, jeuri wala usiwe  na choyo, chuki na hasira  na yote ni lazima wewe pia uwathamini.
Chanzo :Mwananchi

No comments:

Post a Comment