Chama cha CUF visiwani Zanzibar
kimewataka wananchi visiwani humo kupuuza wito wa chama tawala Chama Cha
Mapinduzi (CCM) wa kuwataka wazanzibari wajiandae kwa marudio ya
uchaguzi visiwani humo.
Mwandishi wa BBC Sammy Awami anasema kuwa
CUF anasema kwamba wito wa CCM juu ya maandalizi ya uchaguzi wakati
bado vikao vya usuruhishi wa mgogoro huo bado vinaendelea, ni
kuwachanganya wananchi juu ya nini hasa hatma ya mgogoro wa kisiasa
visiwani humoKwa muda wa zaidi ya mwezi mmoja sasa, viongozi wa juu wa serikali na vyama, ikiwa ni pamoja na marais wastaafu wamekuwa wakiendelea na vikao vya siri vinavyolenga kutafuta suluhu la mgogoro huo wa kisiasa visiwani Zanzibar
Akizungumza na waandishi wa habari mapema leo, Kaimu mkurugenzi wa habari na mawasiliano wa CUF Ismail Jussa amesema
ni vema ikasubiriwa taarifa rasmi ya maafikiano ya vikao vinavyoendelea ambayo bado haijatolewa''
Tangu kufutwa kwa uchaguzi visiwani Zanzibar, chama tawala CCM kiliunga mkono kurudiwa kwa uchaguzi huku CUF ikiapa kuususia uchaguzi huo na kutaka aliyekuwa mgombea urais wake Maalim Seif Sharif Hamad atangazwe kuwa mshindi wa uchaguzi huo, ambao CUF inadai Maalim Seif alishinda kwa asilimia zaidi ya 50%.
Wanaohusika katika msururu wa vikao vya mashauriano ya mgogoro wa Zanzibar ni pamoja na Rais wa Zanzibar Dokta Ali Mohamed Shein, ambaye ndiye mwenyekiti huku wajumbe wakiwa ni makamu wa pili wa rais balozi Seif Ali Iddi, marais wastaafu Amani Abeid Karume, Jakaya Mrisho Kikwete, Ali Hassan Mwinyi, Dokta Salmin Amour Juma na makamu wa kwanza wa rais Maalim Seif Sharrif Hamad ambaye ndiye mwakilishi kutoka upande wa CUF.
Zanzibar iliingia katika mgogoro wa kisiasa miezi miwili iliyopita baada ya mwenyekiti wa tume ya uchaguzi visiwani humo Jecha Salim Jecha kufuta matokeo ya uchaguzi kwa kile alichokiita ukiukwaji wa sheria na utaratibu wakati wa zoezi la upigaji kura.
No comments:
Post a Comment