Tuesday 16 February 2016

Uchaguzi Uganda umefikia hapa


Rais wa Uganda Yoweri Museveni amesema ana imani atashinda urais kwenye uchaguzi mkuu utakaofanyika Alhamisi wiki hii.
Hata hivyo, amesema yuko tayari kukabidhi madaraka kwa mtu mwingine iwapo chama chake kitashindwa.
Akijibu maswali ya mwandishi wa BBC Zuhura Yunus wakati wa kikao na wanahabari ikulu Jumapili, Bw Museveni alisema kwa sasa haoni chama chochote ambacho kinaweza kuondoa chama cha National Resistance Movement (NRM) uongozini.
“Sidhani vyama vya upinzani vitashinda NRM. Kwa sababu tunajua nguvu yetu. Tunajua tutashinda, lakini kama itakuwa tumeshindwa basi tutawaachia wale ambao wameshinda. Lakini sidhani kuna chama kinaweza kushinda NRM wakati huu,” alisema.
Kuhusu kuandaa mtu atakayemrithi muda wake wa kuondoka uongozini ukifika, Bw Museveni alisema hawezi kuandaa mrithi.
“Nimeandaa mrithi kwa shamba langu, lakini sio kwa Uganda. Uganda hawa watu watachagua nani atawaongoza wakati mimi nimestaafu,” alisema.
 
 Hata hivyo hakueleza ni lini atastaafu akisema “raia” ndio watakaomwamrisha kustaafu.
Alidokeza hata hivyo kwamba atatii katiba.
Kwa sasa katiba inaweza umri wa juu zaidi wa rais kuwa miaka 75. Kwa sasa Bw Museveni anakaribia kutimiza umri wa miaka 72 maana kwamba mwaka wake wa mwisho wa muhula ujao, iwapo ataingia madarakani, atakuwa na umri wa miaka 76.
Barani Afrika, viongozi wa mataifa mengi wamekuwa wakifanyia mabadiliko katiba kuwawezesha kuendelea kuongoza.
Nchini Uganda, kulikuwa na kipimo cha mihula miwili kwa rais kuanzia 1996 lakini viliondolewa 2005 na kumuweza Bw Museveni kuwania kwa muhula wa mwingine baada yake kuhudumu kwa mihula miwili.

No comments:

Post a Comment