Saturday, 30 April 2016

Kauli ya Waziri Dk.kigwangwalla kuhusu Maandalizi muswada wa sheria ya wazee hii hapa


Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla
Serikali imekamilisha mapendekezo ya uundwaji wa Sheria ya Wazee ambayo itawasilishwa katika mkutano wa Bunge wa Septemba.

Taarifa hiyo imetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Hamisi Kigwangalla wakati akitoa ufafanuzi kwa Viongozi wa Mtandao wa Wazee waliomtembelea Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ofisini kwake mjini Dodoma.

Dk. Kigwangalla alisema kuwepo kwa Sheria ya Wazee kutawezesha mambo mbalimbali yanayohusu wazee kutekelezwa kwa mujibu wa sheria hiyo likiwemo suala la pensheni.

“Mimi pamoja na Waziri wangu, Ummy Mwalimu baada ya kupewa jukumu la kuongoza wizara tuliunda kikundi cha wazee kwa ajili ya kuamua mambo makubwa mawili ambayo tutayatekeleza likiwemo la pensheni kwa wazee wote,” alisema.
Naibu Waziri huyo alisema suala jingine ambalo wamepanga kulitekeleza ni utoaji wa huduma ya bure kwa wazee, ambapo watawapatia bima ya afya ili wasiendelee kusumbuka.

Kwa upande wake Waziri Mkuu aliwahakikishia wazee hao kwamba Serikali inawatambua na ndiyo sababu ya waliamua wawe na sehemu ya kufikishia malalamiko yao ambayo ni Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto .

Kuhusu ombi la wazee hao kwa Rais Dk. John Magufuli la kuwa na uwakilishi Bungeni kwa kupitia nafasi zake 10 za uteuzi, Waziri Mkuu alisema amelipokea na atalifikisha kwa Mhe. Rais.

Pia amewataka wapanue taasisi yao na kuimarisha mtandao uweze kujulikana na wazee wengi zaidi, wawe na viongozi kuanzia ngazi za vijiji ambapo Serikali ipo tayari kushirikiana nao kwa karibu.

No comments:

Post a Comment