Saturday, 30 April 2016

Mapya yaibuka kuhusu akaunti za Escrow TPDC yasema haya


Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio

Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania, TPDC limetoa ufafanuzi kuhusiana na taarifa kuhusu shirika hilo kufungua Akaunti za ESCROW katika Benki ya Stanbic.

Taarifa kwa umma iliyotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, imesema kuwa Akaunti ya ESCROW ni Akaunti maalumu inayoweza kufunguliwa baina ya kampuni, taasisi, au mashirika mbalimbali ya binafsi na yale ya umma kwa matumizi maalumu. 

Taarifa hiyo imeendelea kufafanua maana halisi ya akaunti ya ESCROW kuwa lengo lake ni kuhifadhi fedha au kupitisha malipo kwa ajili ya shughuli maalum ikiwemo miradi au kazi yoyote maalumu na malipo haya hufanyika baada ya pande mbili kuridhia. 

Ukizungumzia akaunti ambazo zimezua utata, taarifa hiyo imeeleza kuwa TPDC ilifungua akaunti tatu za Esrow baada ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kutoa idhini kufunguliwa kwa akaunti kwenye Benki ya Stanbic, ikiwa ni moja ya masharti yaliyowekwa na mkopeshaji ili kutoa mkopo kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu mipya ya gesi asilia, kutoka Benki ya Exim ya China.

Mkopeshaji alipendekeza Akaunti hizo zifunguliwe kwenye benki ya Stanbic na ambapo taratibu za manunuzi zilizingatiwa, ikiwemo ushindanishaji wa watoa huduma. 

Taarifa hiyo imezitaja akaunti hizo tatu zilizofunguliwa ni pamoja na:
Akaunti hizo tatu zilizofunguliwa ni pamoja na:
1. Akaunti ya Mapato ya Gesi
Lengo la akaunti hii ni hifadhi mapato yote yatakayo tokana na mauzo ya gesi kwa njia ya bomba jipya.


2. Akaunti ya Uendeshaji
Akaunti hii ina jukumu la kuhifadhi fedha zinazohitajika kwa ajili ya shughuli za uendeshaji wa mradi wa miundombinu hiyo mipya ya gesi asilia.


3. Akaunti ya Kulipia Deni
Akaunti hii imefunguliwa kwa ajili ya kulipa madeni yatokanayo na mkopo.


Akaunti hizi zinadhibitiwa na masharti yaliyowekwa kwenye makubaliano (Mkataba) ya Menejimenti ya Akaunti hizo yaliyosainiwa kati ya Benki ya Stanbic (kama Benki ), TPDC (kama mtumiaji wa mwisho), Benki ya Exim ya China (kama Wakopeshaji) na Wizara ya Fedha (kama mdeni kwa niaba ya Serikali ya Tanzania).
TPDC imesema kuwa baada ya taratibu zote hizo kufuatwa, si sahihi kuuhusisha mchakato huu na tuhuma zozote na ukiukwaji wa sheria za nchi. 

Mwisho, taarifa hiyo imesisitiza kwamba Akaunti ya ESCROW ni akaunti ya kawaida kabisa katika utekelezaji wa miradi kama huu wa gesi asilia.

No comments:

Post a Comment