Friday, 29 April 2016

Majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta waanza Tazama hapa

Waziri wa Nishati wa Uganda Bi. Irene Muloni pamoja na timu ya wataalamu wa wizara yake wapo nchini kwa ajili ya mkutano wa kwanza wa majadiliano ya utekelezaji wa mradi wa bomba la mafuta linalotarajiwa kujengwa kutoka nchini humo hadi jijini Tanga.

Bomba hilo litakalojengwa kwa ushirikiano baina ya serikali za Uganda na Tanzania, awali lilikuwa lipitie nchini Kenya na litakuwa likisafirisha mafuta ghafi kutoka eneo la magharibi mwa Uganda mahali ambako imegundulika hazina kubwa ya nishati ya mafuta.

Mwenyeji wake, Waziri wa Nishati na Madini wa Tanzania Profesa Sospeter Muhongo amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo kuwa mbali ya bomba la mafuta, mkutano huo unaohusisha wataalamu kutoka nchi zote mbili, utajadili pia ujenzi wa bomba la kusafirishia gesi kutoka Tanzania kwenda nchini Uganda.

Kwa mujibu wa Profesa Muhongo, bomba la gesi litatumika pia kupeleka nishati hiyo katika mikoa ya kanda ya ziwa, kwa kutumia michoro na miundombinu itakayopita kwenye eneo lile lile ambako bomba la mafuta litajengwa. 

Kwa upande wake, Waziri Muloni amesema Tanzania ni mshirika muhimu katika mradi huo wa ujenzi wa bomba hilo la mafuta linalotarajiwa kukamilika mwaka 2020.

Waziri Muloni ameongeza kuwa wao kama serikali ya Uganda wameridhishwa na utayari wa serikali ya Tanzania wa kuwa mbia na hatimaye kumiliki hisa katika mradi wa ujenzi wa mtambo wa kusafishia mafuta utakaojengwa eneo la Hoima na ambao utasafisha za kuzalisha bidhaa za petroli kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchini Uganda.

No comments:

Post a Comment