Sunday 24 April 2016

Kauli ya Waziri wa Fedha kuhusu watafunaji wa fedha za bajeti hii hapa

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amesema Serikali ya Awamu ya Tano haitawavumilia watafunaji wa fedha za bajeti ya maendeleo.
Kabla ya kuuzindua mwongozo huo, Dk. Mpango alisema Serikali ya Awamu ya Tano inatambua miradi mingi ya maendeleo nchini imeshindwa kutekelezwa kutokana na uwapo wa 'mchwa' waliokuwa wanatafuna fedha za miradi hiyo.
"Mwongozo huu hi muhimu kushawishi wafadhili kuwekeza kwenye miradi ambayo imeandaliwa vizuri. Utaisaidia serikali kupambana na 'mchwa' wanaotafuna fedha za maendeleo kupitia utaratibu wa 'white elephant' (miradi hewa)," alisema.
Dk. Mpango aliendelea kueleza kuwa Serikali ya Awmu ya Tano itahakikisha inausimamia vyema mwongozo huo na mtendaji yeyote wa serikali atakayeshindwa kuandaa na kusimamia miradi mizuri ya maendeleo atashughulikiwa.
"Tunataka tuwe na miradi mizuri inayosimamiwa na kutekelezwa kwa ufanisi, wale watakaoshindwa kufuata utaratibu huu, tutawatumbua," alisema zaidi.
Serikali chini ya Rais wa Tano, John Magufuli imejikita katika kupiga vita rushwa kubwa na ubadhirifu wa fedha za umma tangu kuapishwa kwake Novemba 5, mwaka jana.
Katika kuonyesha dhamira hiyo, Rais Magufuli alitengua uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Dk. Edward Hoseah Desemba 16, mwaka jana kutokana na kutorishwa na namna taasisi hiyo ilivyokua ikitekeleza wajibu wake katika kukabiliana na rushwa; hususani kwenye upotevu wa mapato ya serikali katika bandari ya Dar es salaam.
Katibu Mkuu Kiongozi wa wakati huo, Balozi Ombeni Sefue alisema Rais Magufuli alichukua hatua hiyo baada ya kujiridhisha kuwa utendaji kazi wa TAKUKURU chini ya Dk. Hoseah hauwezi kuendana na kazi anayoitaka.
"Eneo mojawapo la upotevu mkubwa wa mapato ya serikali ni Bandarini na Katika Mamlaka ya Mapato Tanzania TRA," alisema Balozi Sefue.
"Hivyo Mheshimiwa Rais amesikitishwa na kitendo cha taarifa za kuwepo kwa vitendo vya rushwa katika eneo hilo kwa muda mrefu lakini kasi ya TAKUKURU kuchukua hatua haiendani na kasi anayoitaka."
Mbali na 'kumtumbua' Dk. Hosea, Rais Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa watumishi kadhaa wa mashirika na wakala za serikali kutokana na tuhuma mbalimbali za kuisababishia nchi upotevu wa mapato au ubadhirifu.
Baadhi ya watumishi hao, wakiwemo wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Shirika Hodhi la Reli (Rahco) na wakala wa Barabara za Mwendo Kasi (BRT) wameshafikishwa mahakamani.
Naye Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango, Florence Mwanri aliyekuwa amefuatana na Dk. Mpango katika hafla hiyo, alisema watahakikisha fedha zote za wafadhili zinapita kwenye mfumo wa bajeti ili iwe rahisi kwao kusimamia matumizi ya fedha hizo.

No comments:

Post a Comment