Wednesday, 20 April 2016

Mikakati ya Muhimbili yaandaa kambi maalumu nchini kote


Screen-Shot-2016-03-15-at-3.54.41-PM
Watoto takribani 4000 huzaliwa na vichwa vikubwa na mgongo wazi kila mwaka lakini wazazi wenye ujasiri na uelewa takribani 400 tu ndio ambao huchukua jukumu la kupeleka watoto wao hospitalini kutokana na ughali wa tiba yenyewe ambapo asilimia kubwa ni upasuaji.

Gharama za upasuaji kwa mtoto mmoja ni shilingi za Kitanzania laki saba mpaka milioni moja kulingana na ubora wa vifaa vitakavyotumika kufanya upasuaji, ambapo changamoto kubwa katika suala hilo ni uhaba wa vifaa na madaktari bingwa, ambao kwa nchi nzima wako tisa tu, nane kati yao wakiwa Dar es salaam na mmoja anapatikana katika hospitali ya Bugando iliyo kanda ya ziwa, Mwanza.
Kufuatia hali hiyo, taasisi ya mifupa na upasuaji ya Muhimbili na GSM foundation, wamedhamiria kupeleka kambi za upasuaji nchi nzima ambapo katika awamu ya kwanza, mikoa ya Mwanza, Shinyanga, singida, dodoma na Morogoro ambapo wanatarajiwa kuwaona wagonjwa 800 mpaka 1000 na kufanya upasuaji wa watu 80 mpaka 100.
Timu za madaktari bingwa zitafika mikoa husika, kwanza kutoa mafunzo kwa wahudumu wa afya, ya jinsi ya kumhudumia mtoto mwenye kichwa kikubwa na mgongo wazi lakini pia kufanya upasuaji kwa watoto watakaojitokeza, kuhudhuria tiba zitakazotolewa na madktari hao bure.
Akizungumza katika uzinduzi wa kambi hizo za upasuaji, mkuu wa mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda amepongeza madaktari bingwa kuona umuhimu wa kuvuka mipaka, nje ya mfumo wa kibajeti kusaidia watoto wanaozaliwa na tatizo la kichwa kikubwa na mgongo wazi.
Kufuatia kuanza kwa awamu hiyo ya kwanza Mkuu wa mkoa amekabidhi magari kwa madaktari hao bingwa kwaajili ya kukamilisha zoezi hilo ambapo kambi za upasuaji zitaanzia mkoani Mwanza tarehe 27 mwezi wa 4 mpaka tarehe 30, Mkoani Shinyanga Mei 2 mpaka 4, Singida Mei 6 mpaka 8, Dodoma Mei 10 mpaka 13 na Morogoro Mei 15 hadi 17.

No comments:

Post a Comment