Wednesday, 20 April 2016

Rais MAGUFULI amtumia salamu za rambirambi waziri mkuu wa JAPAN


                           Rais JOHN MAGUFULI

Rais JOHN MAGUFULI amemtumia salamu za rambirambi Waziri Mkuu wa JAPAN, SHINZO ABE kufuatia vifo vya zaidi ya watu AROBAINI vilivyosababishwa na tetemeko la ardhi lililokikumba Kisiwa cha KYUSHU Kusini Magharibi mwa JAPAN.

Tetemeko hilo la ardhi limetokea tarehe 14 mwezi huu na kurudia tena tarehe 16 na kusababisha maporomoko makubwa ya udongo yaliyoharibu na kufunika makazi ya watu na miundombinu ya usafirishaji na mawasiliano.

Katika salamu hizo zilizopitia kwa Balozi wa JAPAN nchini TANZANIA, MASAHARU YOSHIDA Rais MAGUFULI ameelezea kushtushwa na idadi kubwa ya watu waliopoteza maisha katika ajali hiyo mbaya na amempa pole nyingi Waziri Mkuu wa JAPAN Mheshimiwa SHINZO ABE.

Aidha Rais MAGUFULI amewapa pole wote waliojeruhiwa wakati wa maporomoko ya udongo na amewaombea wapone haraka ili waweze kuungana na wananchi wengine wa JAPAN katika shughuli za kila siku za ujenzi wa Taifa.

No comments:

Post a Comment