Umebaki mwezi mmoja tu Rais Magufuli akabidhiwe uenyekiti wa chama hicho na Rais mstaafu wa awamu ya nne ambaye pia ni Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete.
Rais Magufuli atakabidhiwa uenyekiti huo Juni na anatarajiwa kupitisha fagio kama alivyofanya serikalini, kwa kuwafukuza viongozi wenye kashfa za rushwa na uzembe.
Mara kadhaa, Rais Magufuli alinukuliwa akimweleza Mwenyekiti wa CCM, Kikwete kwamba amezungukwa na wanafiki na watu ambao alidhani watamsaidia kwenye chama lakini wamemuangusha.
Katika mchakato wa kuwabaini watumishi hewa unaoendelea nchini, zaidi ya watumishi hewa 7,700 wameshabainika ambao wameisababishia serikali hasara ya zaidi ya Sh. bilioni 7.5.
Rais Magufuli alitoa gizo hilo juzi jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na Wenyeviti na Makatibu wa CCM, Wilaya ya Mikoa yote nchini alipokuwa akiwashukuru kwa kufanikisha Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana.
Alisema tangu kuanza kwa zoezi hilo serikalini watumishi hewa wengi wameshabainika ambao walikuwa wanaisababishia serikali hasara na wameanza kushughulikiwa.
“Naamini kama serikalini kuna watumishi hewa na kwenye chama hawatakosekana," alisema Rais Magufuli huku akitabasamu.
"Naomba Katibu Mkuu na wewe uwatafute walioko kwenye chama.” Alisema mabilioni ya fedha zilizokuwa zikilipa watumishi hewa yangeweza kusaidia kujenga barabara, shule na hospitali lakini zinatafunwa na wachache.
“Kwa hiyo nataka kuwahakikishia wana CCM kuwa, sisi tutandelea kusimama imara, tunataka Tanzania iwe yenye neema, Tanzania tajiri, ila kuna watu wachache, ambao wametumia vibaya nafasi zao kwa kujilipa mishahara hewa,” alisema Rais Magufuli.
Sambamba na hilo, Rais Magufuli aliwataka viongozi na wana CCM kuvunja makundi waliyokuwa nayo wakati wa uchaguzi na kusameheana ili kuanza kujenga nchini.
“Kipindi cha kampeni kimeshamalizika na nashukuru kwa kuniwezesha kuwa Rais, naamini bila nyie nisingefanikisha.
"Ni wazi kuwa kulikuwa na wagombea zaidi ya 30 na isingewezekana kukosekana kwa makundi zaidi ya 30 kwa kila mgombea wanaowaunga mkono.”
Alisema angependa kuona CCM inafukia makaburi yote na kusahau kila aina ya makosa waliyofanyiana wakati wa kampeni ili kuanza kufanya kazi kwa pamoja, kukijenga chama na kuwaletea wananchi maendeleo.
Msimamo huo wa Rais Magufuli ni mpya, hata hivyo, kwani amewahi kusema CCM imejaa watu ndumilakuwili ambao mchana wanakuwa CCM na usiku wanahamia upinzani na kutaka watu hao waondolewe ndani ya chama ili kubaki na watu safi.
“Ni heri kuwa na watu wachache ndani ya chama kuliko kuna na kundi la watu wengi amboa ni wasaliti,” aliwahi kusema Rais Magufuli.
Kumekuwa na hisia kwamba Rais Magufuli atatumia wembe ule ule aliowanyolea viongozi wa serikali kuwanyoa viongozi wa chama ambao wamekuwa wakikitumia chama hicho kwa maslahi binafsi.
Kabla la Rais Magufuli kuingia Ikulu, Katibu Mkuu Kinana, amekuwa akinukuliwa na vyombo vya habari, wakati wa ziara zake za kukijenga chama, akikemea wasaliti wa chama na maovu yanayofanywa hasa watumishi wa serikali hadi kuibua sakata la mawaziri mizigo, pamoja na kuisukuma serikali iwachukulie hatua.
“Ni dhahiri akikabidhiwa chama atapanga safu yake kwa hiyo lazima kutakuwa na sura mpya, usitarajie aendeshe chama kwa kutumia watu wale wale aliowakuta maana Mkapa alipoingia aliweka watu wake, Kikwete naye alipoingia alifanya hivyo hivyo kwa hiyo hata Magufuli ataweka sura mpya,” kilisema chanzo kimoja ndani ya CCM.
No comments:
Post a Comment