Sunday 17 April 2016

Waziri Mwigulu atoa kauli hii baada ya Upotevu wa machine ya kusagia taka

 nchemba
Baada ya kuwepo upotevu wa Mashine ya Kusagia taka na kuchemshia Maji, kwa ajili ya matumizi ya Wafanyabiashara na wateja wa Soko la Kimataifa la Kirumba, Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi imeiagiza kamati ya ulinzi na Usalama ya wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza kuchuguza upotevu huo.
Waziri mwenye dhamana katika Wizara hiyo Mwigulu Nchemba, ametoa agizo hilo baada ya kukamilisha ziara ya kutembelea Soko hilo, iliyohusisha ukaguzi wa mazingira ya usafi wa soko, Madaraja ya vivuko vya kusafirishia na kushushia mizigo pamoja na ukaguzi wa barabara, ambapo hatua hiyo ilipokamilika akapokea kilio hicho kutoka kwa Wafanyabiashara.

Ziara ya Soko hilo ilipokamilika Waziri huyo akatembelea Kiwanda cha Samaki cha Vick Fish na Tanzania Fish (TFP) vilivyopo wilayani Nyamagana mkoani hapa, ambapo ameonyesha kuridhishwa na utendaji wa shughuli za viwanda hivyo, ingawa changamoto inayovikabili ni uhaba wa Samaki, hatua inayosababisha wafanyakazi kupunguzwa.

Katika ziara hiyo Waziri Nchemba ameweka jiwe la msingi la kiwanda cha kuchakata Nyama cha Chobo kilichopo wilayani Misungwi na kuzishauri pia taasisi za fedha kuwapa kipaumbele wawekezaji wa sekta ya MIFUGO na uvuvi, ili waweze kuwasaidia wavuvi pamoja na wafugaji kunufaika na shughuli hizo kupitia sekta ya viwanda

No comments:

Post a Comment