Saturday, 21 May 2016

Hii ndio Kauli ya serikali kuhusu hisa za Tanzanite

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama amejikuta akivutana na Mbunge wa Simanjiro, James ole Millya (Chadema), baada ya mbunge huyo kumhusisha na Kampuni ya Sky Associates, inayodaiwa kununua hisa za mgodi wa TanzaniteOne, bila utaratibu.


Mgodi wa madini ya tanzanite kwa sasa unamilikiwa na ubia na Kampuni ya Sky Associates na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kwa asilimia 50 kwa 50.

Akichangia hoja ya bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini bungeni jana, Millya alisema uuzaji wa mgodi wa TanzaniteOne kwenda Kampuni ya Sky Associates ulifanyika kwa hila, hakuna taratibu za zabuni zilizotangazwa nchini na kampuni hiyo ni ya mfukoni ambayo mmoja wa wamiliki ni shemeji wa Mhagama.

“TanzaniteOne iliuzwa bila kufuata taratibu. Stamico na Sky- Associated mkataba wake hauko wazi. Kuna watu wamehusika. Wengine wanasema nisiwataje. Ngoja niwataje. Simbachawene (George) anahusika katika hili. 

“(Simbachawene akiwa Waziri wa Nishati na Madini), aliruhusu ubia katika Serikali bila ya kuwapo kwa ushindani. Wanasema zabuni imetangazwa London Stock Exchange. Sasa huko Watanzania wanahusikaje,” alihoji mbunge huyo.

Kauli hiyo ya Millya, ilimuinuia kitini Waziri Jenista aliyetoa taarifa kuwa si kweli kwamba ana uhusiano na mtajwa, kwani jina la Mhagama ni la ukoo na wako watu wengi.

“Mheshimiwa Mwenyekiti, ukoo wetu hauna huyo mtu, hivyo si sahihi kunihusisha na ukoo wetu. Mbunge afanye utafiti,” alisema Jenista na kuongeza kuwa atachukua hatua zaidi za kikanuni, kama mbunge huyo ataendelea kumhusisha naye.

Lakini licha ya kupewa taarifa hiyo, Millya aliendelea kudai mbia huyo ana uhusiano na waziri huyo na hali hiyo ikamlazimu Jenista kusimama tena baada ya mbunge huyo kumaliza kuzungumza na kueleza kuwa, kwa kutumia Kanuni za Kudumu za Bunge Ibara za 63, 64 na 68, anataka mbunge huyo athibitishe madai yake hayo au achukuliwe hatua.

“Kumezuka tabia ya kuchafuana majina humu ndani kwa kusema mambo yasiyoruhusiwa. Hivyo naomba Bunge lako limtake Mbunge athibitishe madai hayo ili kuondoa mambo haya ya kupakaziana, au la, nichukue hatua zaidi kwa mujibu wa Kanuni,” alieleza Jenista ambaye aliahidiwa kuwa muongozo huo umechukuliwa na utajibiwa baadae na Bunge.

Awali, katika mchango wake, Millya alisema licha ya kuwapo kwa migodi ya Tanzanite wilayani Simanjiro, wananchi wake ni masikini na wawekezaji wameshindwa kusaidia huduma za kijamii.

Kwa upande wake, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema), ametaka kuwapo kwa suluhisho la mgogoro wa muda mrefu kati ya wawekezaji wa mgodi wa Acacia North Mara na wananchi wa eneo la Nyamongo wilayani Tarime.

Ametaka kukomeshwa kwa mauaji ya wananchi, na kwamba njia pekee ya kumaliza tatizo hilo ni kuwapa wananchi eneo la kuchimba dhahabu.

No comments:

Post a Comment