Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watu wenye Ulemavu wa Ngozi- Under The Same Sun, limetoa rai kwa mataifa ya Malawi, Msumbiji na Tanzania kuchukua hatua za haraka za kukomesha biashara ya viungo vya watu wenye ulemavu wa Ngozi, ambayo inadaiwa kuanza kushamiri kwenye mataifa hayo.
Kwa mujibu wa Shirika hilo, nchini Tanzania matukio ya mauaji na biashara ya viungo vya watu wenye albinism yamepungua, lakini nchini Malawi na Msumbiji matukio ya kihalifu na mauaji yameongezeka kwa kasi, na hivyo kuzua shaka kuwa wauaji hao sasa wamehamia kwenye nchi hizo kwa ajili ya kufanya biashara ya Viungo vya watu wenye Albinism
Shirika la Under The Same Sun Limedai ripoti za kiuchunguzi toka kwa watu waliokamatwa kwenye matukio ya kihalifu ya mashambulizi ya watu wenye ualbino, zimeonyesha baadhi yao wamekiri wametumwa viungo hivyo na watu toka nchini Tanzania.
Mwanzilishi na Afisa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Under The Same Sun Bw Peter Ash na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo Tawi la Tanzania, Vicky Ntetema wamebainisha kuwa washirika wao nchini Malawi wamesharikodi matukio ya 65 ya mashambulio kwa watu wenye ulemavu wa ngozi tangu desemba 2014
Katika matukio hayo , watu 13 wenye ulemavu wa ngozi waliuawa, 5 walipotea na 47 walifanyiwa majaribio ya kuvamiwa kwa ajili ya kukatwa viungo vyao.
Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Watu wenye Ulemavu wa Ngozi Under The Same Sun tangu Januari 2015 hadi januari 31 2016, jumla ya watu wanane wenye ulemavu wa ngozi walishambuliwa na kukatwa viungo vyao kwenye mikoa mbalimbali nchini Tanzania.
Hali ya ualbino hutokana na upungufu ama ukosekanaji kabisa wa kiasi fulani cha protini katika mwili ambacho kinahitajika katika utengenezaji wa rangi ya ngozi, wataalam huita – melanin. Ualbino huweza kuwakumba binadamu, wanyama na mimea.
No comments:
Post a Comment