Saturday 14 May 2016

Hizi ndio pesa zilizokusanywa baada Watumishi hewa kuanza kurudisha.

 Wakati operesheni ya kuondoa wafanyakazi hewa kwenye malipo ya mishahara ya serikali na halmashauri ikiendelea nchini

watumishi hewa 16 wameanza kurudisha fedha walizokuwa wakipokea katika halmashauri ya manispaa ya kinondoni.

Taarifa zinaonyesha watumishi hewa katika wilaya hiyo wameongezeka kutoka 89 hadi kufikia 103 na wameipotezea serikali zaidi ya Sh. bilioni 1.2.
Mpaka sasa Sh. milioni 94 zimeshakusanywa kutoka kwa watumishi hewa ambao ni walimu nane wa shule za Msingi, watatu wa shule za Sekondari na watatu wa sekta ya afya, alisemwa jana Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Ally Hapi.

“Baada ya kupitisha msako wa kutafuta watumishi hewa katika Wilaya yangu, tumepata watumishi wengine 14 na idadi imeongezeka, pia kati ya watumishi hao, 16 wameshalipa fedha walizokuwa wakizipokea kama malipo hewa,” alisema.

Alisema watumishi hao ni wale waliosakwa baada ya kubainika kupokea mishahara hewa ambapo walikubali kulipa fedha hizo kwa hiyari.

“Tatizo la watumishi hawa hewa (waliogundulika) haliko Wilaya hii tu, bali wametapakaa maeneo mbalimbali. Wengine wako mikoa mingine kabisa, hivyo tunaendelea kuwasaka na hatua kali zichukuliwe dhidi yao,” alisema Hapi.

Alisema wapo watumishi wengine ambo waliaga kwenda kusoma lakini walipotafutwa kwenye vyuo walikosema wanasoma hakuna taarifa zao.

“Tunashirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama ikiwamo Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) ambapo tumewakabidhi orodha ya majina ili kubaini watumishi hawa hewa walipo na hatua stahiki zichukuliwe,” alisema.

Kuhusu wanaolipa fedha, alisema watamueleza Rais John Magufuli, kuhusiana na hatua walizozichukua na kwamba fedha hizo zitatolewa maamuzi na ngazi ya juu.

Katika Mkoa wa Dar es Salaam kuna watumishi hewa 248 ambao wameipatia hasara serikali ya Sh. bilioni 3.6 baada kulipwa mishahara.

Jumla ya watumishi hewa 10,295 wamebainika katika maeneo yote nchini, ambao walikuwa wakiligharimu Taifa hasara ya Sh. bilioni 11.6 kwa mwezi sawa na Sh. bilioni 139 kwa mwaka.
Kati ya watumishi hao hewa, 8,373 wanatoka Tamisemi na 1,922 wanatoka serikali kuu.

No comments:

Post a Comment