SERIKALI imetangaza kuboresha hospitali za rufaa, maalumu, za kanda na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambayo sasa itaanza kutoa huduma ya kupandikiza figo. Aidha, itajenga jengo maalumu la kulaza viongozi wa kitaifa na watu mashuhuri.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema hayo bungeni mjini hapa jana alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa mwaka wa fedha 2016/2017.
Alibainisha kuwa maboresho hayo kwa upande wa MNH ni pamoja na kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) kutoka 21 hadi vitanda 75.
Pia itanunua vifaa tiba vya upasuaji na kuongeza vyumba vya upasuaji kutoka 13 vya sasa hadi 18, itapanua huduma za kusafisha figo kwa kuongeza vitanda kutoka 15 hadi vitanda 50 na kuanza kusafisha figo kwa wagonjwa wenye Virusi Vya Ukimwi na virusi vya ini.
“Muhimbili itaanzisha huduma mpya ya upandikizaji figo na upandikizaji wa ‘cochlea’ kwa wagonjwa ambao ni viziwi…itajenga jengo la kisasa kwa ajili ya kutoa huduma kwa wagonjwa binafsi na viongozi wa kitaifa na watu mashuhuri litakalokuwa na vitanda 170 na kuongeza mapato kutoka shilingi bilioni 2.6 za sasa hadi shilingi bilioni tano kwa mwezi,” alisema Ummy.
Alisema Taasisi ya Mifupa Muhimbili (MOI) katika mwaka wa fedha 2016/2017, itaongeza nafasi ya wagonjwa wanaolazwa kutoka vitanda 150 hadi 340 ambapo katika chumba cha wagonjwa wenye kuhitaji uangalizi maalumu (ICU) vitaongezeka kutoka vinane hadi 32.
“Serikali itanunua mashine mpya za uchunguzi ikiwa ni pamoja na MRI, CT scan na Xray za dijitali. MOI itatoa mafunzo na upasuaji wa marejeo kwa nyonga na goti,” alifafanua.
Kwa upande wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete ambayo mwaka wa fedha 2015/2016 ilihudumia wagonjwa 24,570 wa nje na waliolazwa 2,134, alisema katika mwaka ujao wa fedha wizara itaijengea uwezo taasisi hiyo kwa kuweka vifaa ili chumba cha upasuaji cha tatu kianze kufanya kazi.
Waziri huyo alisema huduma za kibingwa za mkoba (outreach services) zitatolewa katika hospitali za Temeke, Amana, Mwananyamala (zote za Dar es Salaam), Tumbi mkoani Pwani na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro.
Kwa upande wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, alisema katika mwaka wa fedha 2016/2017 itapatiwa vifaa vya kisasa vya uchunguzi na matibabu ikiwa ni pamoja na PET/CT scan, Linac na MRI.
Pia itatoa huduma za mkoba hasa katika maeneo yatakayoonekana kuwa na idadi kubwa ya wagonjwa wenye saratani. “Wizara itaimarisha upatikanaji wa dawa kwa wagonjwa wa saratani ambapo asilimia 13 ya fedha za dawa zitatumika kununua dawa za saratani ili kupunguza mzigo kwa wagonjwa hasa wa kipato cha chini,” alisema.
Kuhusu Hospitali ya Mirembe, alisema mafunzo yatatolewa kwa watumishi ili kukidhi mahitaji ya kutoa huduma kwa waathirika wa dawa za kulevya na kwa Hospitali ya Bugando kutafungwa CT scan simulator kwa ajili ya kupanga matibabu na mashine mbili za Varian & Elekta linac kwa ajili ya matibabu ya saratani.
Hiyo itasaidia matibabu ya mionzi kutolewa Mwanza badala ya wagonjwa kwenda Dar es Salaam. Ummy alisema katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC itafungua wodi mpya za wagonjwa walioungua kwa moto na kemikali na kuanzisha Kitengo cha ICU kwa ajili ya watoto na kununua vifaa vya uchunguzi vya CT Scan, MRI pamoja na vifaa kwa ajili ya jengo jipya la huduma za dharura.
Katika hatua nyingine, waziri amesema serikali imebaini vituo vya afya 73 kati ya 5,235 vilivyopo nchini ndivyo vyenye hadhi ya kuwa vituo vya afya. Waziri akizungumzia tathmini ya vituo vya afya 5,235, alisema kati yake vituo 2,016 sawa na asilimia 38.51 vimepata nyota 0, vituo 2,583 vimepata nyota moja, vituo 561 vimepata nyota mbili.
Nyota hizo zote kuanzia sifuri hadi mbili maana yake havistahili kuwa vituo vya afya. Ni vituo 68 vilivyopata nyota tatu na vituo vitano vimepata nyota nne yaani ndiyo vyenye sifa ya kuwa vituo vya afya.
Alisema lengo la serikali ni kuhakikisha asilimia 80 ya vituo vilivyofanyiwa tathmini vinapata nyota tatu na zaidi ifikapo Juni mwaka 2018. Alisema wizara inaangalia uwezekano wa kurekebisha sheria ili kufuta matangazo ya tiba asili na tiba mbadala.
Alisisitiza kwa wamiliki wa vyombo vya habari kuhakikisha matangazo yote ya tiba asili na tiba mbadala yanayotolewa kwenye vyombo vya habari yameidhinishwa na Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala.
Alisema Taasisi ya Taifa ya Utafiti ya Magonjwa wa Binadamu (NIMR) kwa kushirikiana na kikundi cha kudhibiti Ukimwi Tanga (TAWG) itafanya majaribio juu ya ubora na usalama wa dawa ya asili aina ya Tashack ya tiba ya Ukimwi ambayo imeboreshwa na kutengenezwa kiwandani.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii kuhusu utekelezaji wa bajeti ya wizara hiyo iliyoomba kuidhinishiwa Sh 845,112,920,056, Peter Serukamba ameomba serikali kufanyia uchunguzi ongezeko la gharama kwa baadhi ya maeneo kwa zaidi ya mara 10 katika ujenzi wa jengo la ghorofa saba la MOI kwa ajili ya kutolea huduma za uchunguzi ikiwemo CT Scan, MRI, Xray, Ultra Sound, ICU, vyumba vya wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu na vyumba vya wagonjwa wa kulipia na kuchangia.
Jengo hilo lililokamilika kwa asilimia 95, litakapokamilika litatumia Sh bilioni 27.23 ambazo ni mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).
No comments:
Post a Comment