Monday 2 May 2016

Miaka 30 jela kwa ubakaji mtoto wa miakia saba.

Mahakama ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela mkazi wa kijiji cha Ubaruku wilayani humo Joseph Kawimbe(19) kutokana na kosa la ubakaji wa mtoto mwenye umri wa miakia saba.

Hukumu hiyo imetolewa na hakimu Mfawidhi wa wilaya ya Mbarali Agnes Ringo aliyesema ameridhishwa na ushahidi uliotolewa na upande wa ulalamikaji ikiwemo maelezo ya mtoto aliyetendewa kosa hilo ambaye alionekana kuwa na uwezo mkubwa wa kujieleza mahakamani.

Awali ilidaiwa na mwendesha mashitaka wa Jeshi la Polisi Mazoya Ruchagula kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo Januari 11 mwaka huu majira ya 10:30 za jioni katika kijiji cha Ubaruku wilayani hapa.

Mbele ya hakimu Ringo, mwendesha mashitaka ameeleza kuwa kijana Joseph alimlaghai mtoto huyo akimtaka amsindikize na ndipo alipompakia kwenye baiskeli lakini walipofika eneo la Ujewa Misheni alimpeleka kichakani na kumtendea ukatili huo na kumsababishia maumivu makali.

Amesema mama wa mtoto huyo baada ya kutomwona mwanaye kwa muda mrefu alilazimika kuanza kumtafuta kwa majirani, lakini wakati akiendelea na jitihada hizo alimuona kijana Joseph akiwa amembeba kwenye baiskeli kumrudisha nyumbani na ndipo alipoita majirani na kubaini kuwa alikuwa amemtendea ukatili wa ubakaji.

Kufuatia kitendo hicho mwendesha mashitaka ameiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili kutoa fundisho kwa wengine wenye tabia hizo kutokana na kile alichoeleza kuwa vitendo vya ubakaji vimeshamiri wilayani humo.

Akitoa hukumu hiyo, Hakimu Ringo amesema mshitakiwa anapaswa kutumikia miaka 30 jela kwa kutenda kosa kinyume cha sheria namba 130 kifungu kidogo namba 2(e) na namba 131 ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

No comments:

Post a Comment