Zoezi la majaribio kwa mabasi yaendayo haraka jijini dar es salaam limesogezwa hadi jumatatu ambapo wananchi wataanza rasmi kulipia usafiri huo ikiwa ni ombi la mkuu wa mkoa wa dar es salaam Paul Makonda ili wananchi wapate muda zaidi wa kujifunza kutumia usafiri huo.
Hayo yamebainishwa wakati viongozi mbalimbali wa jiji la dar es salaam walipotembelea mradi huo ili kujionea namna ambavyo unafanya kazi ambapo walipata fursa ya kupanda mabasi hayo kutoka kariakoo-kimara na kuishia morocco.
Aidha makonda ametoa wito kwa wananchi kubadilika kulingana na elimu wanayopata hususan wale ambao bado wanaingilia barabara za mabasi hayo ikiwemo madereva wa bodaboda na magari pamoja na watembea miguu , na kwa wale watakaobainika kuharibu miundombinu hatua kali zitachukuliwa akitolea mfano basi lililogonga kituo kimojawapo cha mabasi hayo cha kimara baruti ambaye anatakiwa kulipa kiasi cha shilingi milioni 200.
Mkurugenzi mtendaji UDA-RT David Mgwassa amebainisha changamoto zilizoibuka katika kipindi hiki cha mpito ikiwemo baadhi ya abiria kutotumia milango maalumu ya kuingilia ndani ya vituo hususan vile ambavyo havijawekewa uzio, jambo ambalo linapoteza mapato lakini pia utaratibu wa abiria kuzunguka na gari muda wote badala ya kupisha wengine watumie huduma hiyo.
No comments:
Post a Comment