Monday 2 May 2016

Tazama Mgomo wa wafanyakazi Kiwanda cha Pepsi (SBC ) jijini Dar es salaam hapa

head-office-img
Wafanyakazi wa Kiwanda cha  Pepsi cha SBC jijini Dar es salaam wamegoma kufanya kazi, wakiushinikiza uongozi wa kiwanda hicho kuongeza mishahara yao,ikiwa ni pamoja na kuboresha mikataba yao kazi ambayo wamedai inawanyanyasa na kuwakandamiza.

Wakizungumza na Channel Ten wafanyakazi hao wamesema wamekuwa wakifanyakazi katika mazingira magumu kwa muda mrefu, huku wakifanya kazi kwa masaa mengi zaidi kwa malipo kidogo ambayo hayakidhi mahitaji yao kimaisha,

Aidha, Wafanyakazi hao wamedai kusikitishwa na hatua ya kiwanda hicho kuweka makampuni ya udalali yanayosimamia wafanyakazi wa kiwanda hicho, badala ya wafanyakazi hao kusimamiwa na SBC, ambapo wamedai makampuni hayo ya udalali yamekuwa yakiwanyanya kwa kutowapa huduma muhimu kama matibabu wakati mfanyakazi anapougua.

Wafanyakazi hao pia wameulalamikia uongozi wa kiwanda cha SBC kwa kuwanyima huduma ya choo vibarua wa kiwanda hicho ambao wamedai kujisaidia nje ya kiwanda, jambo ambalo wameliita ni unyanyasaji unaofanywa na viongozi hao kwa vibarua.

Kufuatia malalamiko hayo, Channel Ten iliutafuta uongozi wa kampuni ya SBC na makampuni ya udalali yanayodaiwa kutumiwa na kiwanda, ambao hata hivyo walikana tuhuma zilizotolewa dhidi yao na wafanyakazi.

Kamanda wa Polisi kanda ya Ilala SACP MKODYA aliyefika kiwandani hapo alibaini kuwepo kwa baadhi ya kasoro zilizofanywa na uongozi huo kuhusu  tuhuma zilizotolewa dhidi yao na wafanyakazi wa kiwanda hicho huku akitaka kasoro hizo zifanyiwe kazi ili kuwepo na maelewano kati ya kiwanda na wafanyakazi wake.

Licha ya Uongozi na Polisi kuwataka wafanyakazi hao kuondoka eneo hilo huku tatizo lao likiendelea kushughulikiwa lakini wafanyakazi hao waliendelea kubaki katika eneo hilo wakiitaka serikali kuingilia kati sakata hilo.

No comments:

Post a Comment